2014-05-06 07:36:32

Utu na heshima ya binadamu dhidi ya ukatili!


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva pamoja na ujumbe wake wanasema kwamba, Vatican inatoa umuhimu wa pekee katika Mkataba dhidi ya ukatili, CAT kama chombo muhimu sana katika mapambano dhidi ya vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Askofu mkuu Tomasi ameyasema hayo siku ya Jumatatu tarehe 5 Mei 2014 alipokuwa anawasilisha taarifa ya Vatican dhidi ya ukatili katika Tume ya Umoja wa Mataifa inayoendelea na kikao chake mjini Geneva. Vatican iliridhia mkataba huu kunako tarehe 22 Juni 2002 ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu mintarafu Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki msingi za binadamu.

Askofu mkuu Tomasi anafafanua kwamba, Vatican kama nchi mwanachama inajikita kwa namna ya pekee katika eneo la mji wa Vatican ambalo inaweza kutekeleza mamlaka yake kisheria, kutokana na ufafanuzi huu, utekelezaji wa mkataba huu hauna budi kuangaliwa mintarafu mji wa Vatican na viunga vyake. Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu umefafanua hatua za kisheria ambazo zimetekelezwa na Mji wa Vatican, kama sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyokuwa yametolewa kwenye mkataba wa kudhibiti ukatili.

Askofu mkuu Tomasi amebainisha kwamba, Vatican haina mamlaka kisheria kudhibiti ukatili unaoweza kufanywa na watoto wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Kila mwamini anayeishi katika nchi fulani anawajibika na kuwajibishwa na sheria za nchi husika. Kutokana na mantiki hii, kila serikali ina wajibu wa kulinda watu walioko chini ya mamlaka yake, kama ilivyo Vatican kuwajibika kwa watu wanaoishi mjini Vatican mintarafu sheria zake.

Askofu mkuu Tomasi anasema, serikali za nchi husika zinawajibika kisheria kuwashughulikia watu wote wanaovunja sheria na kusababisha nyanyaso na dhuluma katika eneo lake. Kila mtu hata kama ni mwanachama wa taasisi zinazosimamiwa na Kanisa Katoliki anawajibika kwa mamlaka halali ya nchi anamoishi.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Silvano Tomasi kwamba, utekelezaji wa mkataba dhidi ya ukatili unazingatia maeneo yaliyobainishwa kwenye mkataba huo na wala si vinginevyo. Hii inatokana na ukweli kwamba, ikiwa kama wanachama wataingiza mambo mengine nje ya mambo msingi yaliyobainishwa kwenye mkataba, watakuwa wanakwenda kinyume cha asili na malengo yake na hivyo kuhatarisha hali ya watu ambao wameteswa na kudhulumiwa. Kwa mantiki hii kazi ya tume itakuwa inaonesha udhaifu mkubwa na hata pengine kukosa uhalali wa kuendelea kuwepo!







All the contents on this site are copyrighted ©.