Sakramenti ya kipaimara hukuza na kuzamisha neema ya Ubatizo!
Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara muungano wa Wabatizwa na Kanisa hufanywa kuwa
mkamilifu zaidi, kwani wanatarajirishwa kwa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu na hivi
hulazimika kwa nguvu zaidi kuieneza na kuitetea imani kwa maneno na matendo, kama
mashahidi wa kweli wa Kristo na Kanisa lake.
Sakramenti
ya Kipaimara hukuza na kuzamisha neema ya Ubatizo kiasi cha kuwafanya Wakristo wathubutu
kumwita Mwenyezi Mungu, “Abba, yaani Baba”. Inawaunganisha zaidi na Kristo na kuwapatia
mapaji ya Roho Mtakatifu ambayo Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuyatafakari katika
katekesi zake za kila Jumatano zinazotolewa mjini Vatican.
Ni Sakramenti inayokamilisha
kiungo cha kanisa na kuwapatia waamini nguvu na neema ya pekee ya kutetea imani kwa
maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo yanayodhihirisha ushuhuda wa imani tendaji.
Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara, waamini wanaweza kukiri kwa ushujaa na ujasiri
mkuu jina la Yesu na kamwe hawawezi kuuonea aibu Msalaba wa Kristo, kielelezo cha
huruma, msamaha na upendo wa Mwenyezi Mungu kwa watu wake.
Wakristo wanaopokea
Mapaji ya Roho Mtakatifu kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara, wanakumbushwa kwamba,
wanapokea mhuri wa kiroho unaowawezesha kuwa na: roho wa hekima na akili; roho wa
ushauri na nguvu; roho wa elimu na ibada pamoja na roho wa uchaji mtakatifu. Hivi
ndivyo Askofu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Katoliki Mbulu anavyowafundisha waamini wake
116 kutoka Parokia ya Roho Mtakatifu, Jimbo Katoliki la Mbulu wakati alipokuwa anatoa
Sakramenti ya Kipaimara hivi karibuni Parokiani hapo.
Askofu Beatus Kinyaiya
alitumia fursa hii kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kanisa la Parokia ya Roho Mtakatifu,
utakaogharimu kiasi cha shilingi za kitanzania millioni 915 hadi utakapokamilika.
Askofu
Kinyaiya anaendelea kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini
Tanzania kusali kwa ajili ya kuombea ufanisi na tija katika vikao vya Bunge Maalum
la Katiba ili wajumbe waweze kutekeleza dhamana nyeti waliyotumwa kuifanya na watanzania
wenzao walipowachagua kuwawakilisha Bungeni. Askofu Kinyaiya anasema, watanzania wengi
hawafurahii kuona wala kusikia malumbano yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi
na maendeleo ya watanzania wote.
Kuna haja kwa Wabunge kubadilika na kuanza
kuonesha dira na mwelekeo mpya katika mijadala ya kutunga Katiba mpya ya Tanzania.
Watanzania wanahitaji mambo makuu matatu kwa sasa: Katiba Mpya itakayolinda: amani,
umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa ajili ya ustawi na maendeeleo ya watanzania wote.
Watanzania wanahitaji Katiba ambayo kimsingi ni sheria mama itakayowaongoza katika
mchakato wa maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Katiba itakayolinda na kudumisha
haki msingi, utu na heshima ya binadamu pamoja na uhuru wa kuabudu.