2014-05-06 11:55:47

Madhulumu ya Wakristo ni chachu ya utakatifu!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake Jumanne, tarehe 6 Mei 2014 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican amewataka waamini kutolea ushuhuda wa imani tendaji na uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Mama.

Baba Mtakatifu amesimulia safari ya ushuhuda iliyooneshwa na Mtakatifu Stefano, shahidi wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya imani kwa Kristo na Kanisa. Ni ujasiri na ushujaa uliopelekea wivu kutoka wakuu wa Makuhani na waandishi hata wakamtwanga kwa mawe hadi kufa! Ni kundi la watu lililokuwa linapingana na Roho Mtakatifu kwani ndani mwao walikosa amani na utulivu na matokeo yake, mioyo yao ilisheheni wivu na roho mbaya, matunda ya kazi ya Shetani katika maisha ya mwanadamu!

Kifodini cha Stefano kinaonesha mapambano kati ya Mungu na Shetani na kwamba, Wakuu wa makuhani walipania kuwadhulumu wafuasi wa Yesu ambao tayari walikuwa wamekwisha ambiwa na Yesu mwenyewe kwamba, wangekumbana na madhulumu kwa ajili ya jina lake, lakini walikuwa hawana sababu ya kusikitika, kwani kwa mwamini kuyamimina maisha yake ni sehemu ya mchakato wa kumwilisha Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Yesu. Madhulumu yakipokelewa kwa imani ni chemchemi ya utakatifu ndani ya Kanisa na kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, wao ni wafuasi wa Kristo, wanaotakiwa kutolea ushuhuda wa imani tendaji katika maisha yao hata kama itawabidi kujisadaka kwa kuyamimina maisha yao! Baada ya mauaji ya Stefano shahidi, Kanisa lilikumbana na mkono wa chuma, kiasi cha kuwasambaratisha Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Walidhani kwa kufanya hivi walikuwa wanazima moto wa Injili, lakini kumbe sivyo!

Wakristo kila walipofika waliendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa hakika, damu ya Mashahidi imekuwa ni mbegu ya Ukristo sehemu mbali mbali za dunia. Kuna haja kwa Wakristo kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa, kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu anaendelesa kufanya kazi ndani ya Kanisa.

Kwa njia hii, Kanisa lina uhakika wa kutembea katika njia ya ukweli na haki, kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha, yaani ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wakristo wanapofanya tafakari kuhusu ushuhuda wa imani ulioneshwa na Stefano pamoja na Wakristo waliokuwa wanakimbia mateso na madhulumu wanapaswa kuchunguza dhamiri zao ili kutambua hali yao ya maisha ya kiroho, kama kweli inazaa matunda yanayokusudiwa, yaani wongofu wa ndani na ushuhuda wa maisha kama njia sahihi ya kumwilisha wito na maisha ya Kikristo!







All the contents on this site are copyrighted ©.