2014-05-05 11:45:38

Utukufu na sifa; uchu wa mali na madaraka ni kikwazo katika kufuasa Kristo!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 5 Mei 2014 anasema, kwa bahati mbaya ndani ya Kanisa kuna watu wanaomfuata Yesu kwa sababu zao maalum: kuna wale wanaotafuta utukufu na sifa mbele ya watu; kuna wale ambao wana uchu wa mali na madaraka na wengine ni wale wanaojikita katika upendo thabiti, wote hawa wanapaswa kuomba neema ili kuwa kweli ni wafuasi aminifu wa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu ameyasema hayo akirejea katika Injili ambamo kundi kubwa la watu linamtafuta kwa sababu lilikula na kusaza, linapokutana na Yesu kwa mara ya pili, Yesu anawachangamotisha kubadilika kwa kujikita zaidi katika wongofu wa ndani na maboresho ya maisha ya kiroho. Ufuasi wa Kristo si kwa ajili ya kujionesha mbele ya watu, kutafuta utukufu na sifa bali ni katika hali ya unyenyekevu na upendo wa dhati.

Haya ni mambo ambayo yamejionesha hata miongoni mwa Mitume wa Yesu na wanaanza kupata mabadiliko ya ndani pale wanapompokea Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anasema, licha ya waamini kupata neema ya ubatizo, lakini bado wanaweza kutawaliwa na dhambi, ubinafsi hata uchu wa mali na madaraka, jambo la msingi ni kila mwamini kuchunguza dhamiri yake na kuangalia kama anamfuasa Yesu kwa kukumbatia Msalaba!







All the contents on this site are copyrighted ©.