2014-05-05 10:27:13

Ushindi unapatikana kutokana na mateso na Msalaba!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 4 Mei 2014 majira ya asubuhi ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa ajili ya Mama Kanisa kumtangaza Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu, katika Ibada iliyohudhuriwa na waamini wengi kutoka Poland, wanaoishi mjini Roma. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa la Mtakatifu "Stanslao alle Botteghe Oscure".

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amemwonesha Mtakatifu Petro alivyosimama kidete kuwaimarisha ndugu zake katika imani katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kwani walikuwa wamejengwa kwenye msingi thabiti ambao ni Kristo mwenyewe. Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II walikuwa kweli ni miamba wa imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu ameungana na Wakristo kutoka Poland kwa ajili ya kumshukru Mungu kwa zawadi ya Yohane Paulo II aliyesali Kanisa hapo zaidi ya mara themanini katika maisha yake. Alikuwa ni mtu mwenye imani kubwa hata pale matumaini ya watu wengi yalionekana kufifia! Parokia hii imekuwa ni mahali pa kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu; Nyumba ya Sakramenti za Kanisa na faraja kwa maskini. Hapa ni chemchemi ya furaha na Uinjilishaji mpya!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutoka Poland kufuata mfano wa Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kutambua kwamba, wao ni mahujaji wanaotakiwa kuwa ni mashahidi wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo anayeendelea kutembea kando ya wafuasi wake katika hija ya maisha! Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanachota nguvu ya hija ya maisha yao kutoka katika Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu, ili kufungua macho ya imani na kurutubisha matumaini na mapendo, ili kuwaonjesha wengine matumaini na furaha inayobubujika kutoka katika Neno la Mungu.

Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kutoka Poland kwamba, katika historia ya maisha ya nchi yao, wamejaribiwa kiasi cha kutosha na sasa wanafahamu kwamba, ili kupata ushindi, hawana budi kukabiliana na mateso pamoja na Msalaba, huu ndio ushuhuda uliotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II, changamoto na mwaliko wa kuiga mfano wa maisha yake.







All the contents on this site are copyrighted ©.