Tume ya haki na amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, imetoa mafunzo maalum kwa
kikundi cha watu 150 kitakachoshiriki katika kusimamia mchakato wa uchaguzi mkuu nchini
Malawi, unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 20 Mei 2014. Wajumbe hawa wanaotoka katika
Majimbo ya: Karonga, Mzuzu na Dedza, watapelekwa kwenye vituo vya kupigia kura na
wakati wa kuhesabu kura ili kujidhirisha kwamba, uchaguzi mkuu nchini Malawi umefanyika
kwa kuzingatia ukweli, uwazi na uhuru.
Tume ya haki na amani inawahamasisha
waamini na wananchi wote wa Malawi katika ujumla wao kuhakikisha kwamba, wanashiriki
kikamilifu katika mchakato mzima wa uchaguzi, kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana
yao katika maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Wajumbe wametakiwa kuhakikisha
kwamba, wanatumia ujuzi na maarifa waliyopata kutoka katika mafunzo haya, ili kutekeleza
wajibu wao kama wasimamizi wa ndani, katika uchaguzi utakaovishirikisha vyama vikuu
vitatu vya kisiasa nchini Malawi.
Wasimamizi wa ndani waliandaliwa na Tume
ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi wamejengewa uwezo wa kutambua
kinzani za uchaguzi pamoja na kinzani zinazoweza kujitokeza katika utawala na mikakati
iliyowekwa. Wadau mbali mbali watakaopewa dhamana ya kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi
wanapaswa kutekeleza kazi hii kwa weledi na dhamiri nyofu ili matokeo ya uchaguzi
yaweze kupokelewa na wote, tayari kuanza mchakamchaka wa kuwaletea wananchi wa Malawi
maendeleo endelevu.
Wasimamizi wa ndani ni waamuzi wanaotekeleza wajibu wao
kwa niaba ya Tume huru ya uchaguzi nchini Malawi. Usimamizi makini, unaojikita katika
ukweli na uwazi ni msaada mkubwa katika kuwaaminisha wapiga kura na viongozi wao kwamba,
uchaguzi ulikuwa ni wa kweli, haki na uwazi.
Wasimamizi hawa pamoja na mambo
mengine wamewezeshwa katika misingi ya haki na amani, uchaguzi na usimamizi bila
ya kupendelea; changamoto za uchaguzi nchini Malawi kama zilivyobainishwa na Baraza
la Maaskofu Katoliki Malawi.