2014-05-05 08:17:53

Msikate tamaa!


Dr. Olav Tveit Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni amehitimisha hija yake ya kichungaji nchini DRC ambako alipata nafasi ya kuweza kujionea mwenyewe shida na mahangaiko; imani na matumaini ya wananchi wa DRC wanaoendelea kupambana na vita pamoja na kinzani za kijamii. RealAudioMP3
Dr. Tveit amewashirikisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema tafakari ya kina kuhusu umuhimu wa ufufuko wa Yesu Kristo hasa nchini DRC, nchi ambayo imesahaulika na matatizo yake yote kufutika vichwani mwa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa. Mahangaiko na mateso ya wananchi wa DRC kwa sasa si habari yenye mashiko kwani eti ni “majanga” yaliyozoeleka. Lakini ikumbukwe kwamba, hakuna jamii inayoweza kuzoea mateso na mahangaiko yanayosababishwa na vita pamoja na kinzani za kijamii.
Kuanzia tarehe 25 Aprili hadi tarehe 2 Mei 2014, Dr. Tveit na ujumbe wake, wakiwa nchini DRC wamekutana na kuzungumza na waamini pamoja na viongozi mbali mbali wa Makanisa. Mada zilizotawala wakati wa hija hii ya kichungaji ni: haki na amani; usalama na utulivu nchini DRC na Afrika katika ujumla wake mintarafu ufufuko wa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia.
Dr. Tveit amewakumbusha wananchi wa DRC kwamba, ufufuko wa Yesu haukutokea wakati mambo yalipokuwa shwari! Amefufuka kutoka wafu, ili aweze kukutana na kuwaimarisha wale waliokata tamaa, wanaoendelea kukumbana na dhuluma na nyanyaso mbali mbali pamoja na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Ufufuko wa Kristo ni kielelezo cha mwanga mpya unaowaangazia wale wanaotembea katika uvuli wa dhambi na mauti, ili kuona mwanga na kuanza kutembea kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha yao.
Ujumbe wa imani na matumaini ni muhimu sana kwa wananchi wa DRC ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiteseka kutokana na vita isiyokuwa na ukomo nchini humo; vita ambayo imejikita kutokana na utajiri wa rasilimali zilizoko nchini humo, utajiri ambao ungeweza kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa DRC, lakini kwa sasa umekuwa ni chanzo cha mateso na mahangaiko yao: kiroho na kimwili.
Dr. Tveit anawahakikishia kwamba, hata wao Yesu Kristo ameteswa, akafa na kufufuka kwa ajili yao, ili waweze kukombolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti na kwamba, licha ya mateso na mahangaiko yao, iko siku wataona mwanga wa ukombozi ukiwaangazia, hapo ndipo watakapoanza hija ya haki na amani, upendo na mshikamano.
Dr. Olav Tveit na ujumbe wake, walipokuwa nchini DRC wamekutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Makanisa pamoja na wanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Wamesali na kushirikishana imani na matumani katika mahangaiko ya wananchi wa DRC.







All the contents on this site are copyrighted ©.