2014-05-05 09:58:54

Mshikamano wa Papa na wananchi wa Afghanstan na Ukraine


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malkia wa mbingu, Jumapili iliyopita, tarehe 4 Mei 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye katika sala kwa Bikira Maria kwa ajili ya wananchi wa Ukraine ili vita na kinzani za kijamii ziweze kukoma na watu waanze kujikita katika amani na udugu.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka na kuwaombea watu ambao wamefariki dunia hivi karibuni kwa kufukiwa na maporomoko ya udongo huko Afghanistan, ili waweze kuonja huruma ya Mungu na kuwapokea katika amani ya milele. Anapenda kuwatia shime wote waliosalimika katika janga hili kusonga mbele kwa njia ya msaada wa wasamaria wema wanaojitahidi kuwapunguzia mateso na mahangaiko!

Mwishoni, Baba Mtakatifu ameungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika maadhimisho ya siku ya tisini ya Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu yanayoongozwa na kauli mbiu "pamoja na vijana wahusika wakuu kwa siku za usoni". Baba Mtakatifu anasema, anaendelea kukiombea Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu ili kidumu katika uaminifu na utume wake. Panapo majaliwa katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 atatembelea Kitivo cha tiba na upasuaji pamoja na Hospitali ya Gemelli, iliyoko mjini Roma.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wanachama wa "Meter" ambao kwa muda wa miaka ishirini wamekuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea haki msingi za watoto. Amewapongeza pia waamini na watu wote wenye mapenzi mema walioungana katika maandamano ya kutetea zawadi ya maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.