2014-05-05 09:36:46

Mabalozi wa Vatican ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha umoja na udugu


Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 2 Mei 2014 majira ya jioni aliitembelea jumuiya Taasisi ya Kipapa ya Wanadiplomasia wa Kanisa inayoundwa na Mapadre 29 kutoka katika nchi 16, wanaojiandaa kwa ajili ya kutoa huduma ya kidiplomasia kama wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbali mbali duniani.

Baba Mtakatifu alipokelewa na wakuu wa Jumuiya hii pamoja na kusali nao masifu ya jioni, baadaye Baba Mtakatifu alizungumza na wanajumuiya hawa kama Baba na familia yake, akigusia masuala mbali mbali ya maisha na utume wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee umuhimu wa majiundo makini kwa viongozi wa Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu anasema, kwa Mapadre wanaoandaliwa kuwa wanadiplomasia wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia hawana budi kukazia mambo makuu matatu: weledi utakaowawezesha kutekeleza dhamana na majukumu yao kwa ufanisi mkubwa, tija pamoja na kujiamini. Pili hawana budi kujenga na kudumisha udugu unaoimarisha upendo na mshikamano katika maisha ya Kipadre.

Tatu, wajenge utamaduni wa kusali na kufanya tafakari ya kina ya Neno la Mungu pamoja na kudumisha Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu itakayowasaidia kuzungumza na Kristo kwa kumshirikisha matatizo, furaha na changamoto katika maisha na utume wao.

Baba Mtakatifu amewataka Mapadre hawa wanaojiandaa kuwa wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia kujikita katika dhana ya unabii, kwa kuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu kwa kutambua historia ya ukombozi katika Agano la Kale na Agano Jipya, kwa njia hii wataweza kuwatumikia vyema watu wa Mungu kwa nyakati hizi.

Baba Mtakatifu anawataka kuwa makini kwa kusoma alama za nyakati, hali inayowataka kuwa na weledi unaojikita katika ufahamu wa kina wa nchi wanayoitumikia. Ili kuweza kupata ufahamu mkubwa kuna haja ya kujifunza, kutembelea na kuzungumza na wananchi husika. Jambo la tatu kwa wanadiplomasia wa Kanisa ni kutekeleza wajibu wao kwa unyenyekevu.

Baba Mtakatifu Francisko amekazia umuhimu wa wanadiplomasia wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia, ili kujenga na kudumisha umoja, udugu na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Maaskofu mahalia pamoja na kutambua hatari wanazoweza kukumbana nazo wakati wanatekeleza dhamana hii nyeti katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu hata katika medani za kimataifa.

Baba Mtakatifu amegusia pia maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia itakayofanyika mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014. Katika maongezi yake, Papa amewasikiliza kwa umakini mkubwa Mapadre wanaojiandaa kutoa huduma za kidiplomasia sehemu mbali mbali za dunia.








All the contents on this site are copyrighted ©.