Kanisa linaendelea kujizatiti kuwalinda na kuwatetea watoto
Mkutano wa kwanza wa Tume ya Kipapa ya kulinda watoto wadogo iliyokuwa na mkutano
wake wa kwanza kuanzia tarehe 1- 3 Mei, 2014 ulikuwa na dhamana ya kutoa mapendekezo
kwa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu majukumu ya Tume hii pamoja na kuongeza wajumbe
kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kuimarisha mikakati ya Kanisa katika kulinda
na kuwatetea watoto wadogo.
Wajumbe hawa katika tamko lao la pamoja wanapenda
kuonesha mshikamano wao wa dhati na wahanga wa nyanyaso za jinsia na kwamba, tangu
mwanzo wa utume wao, wanapenda kutoa kipaumbele cha kwanza katika kulinda na kutetea
watoto wadogo au watu wazima wakati wa kufanya maamuzi. Wajumbe wamepata fursa ya
kueleza na kushirikisha mawazo, uzoefu na mang’amuzi pamoja na matarajio yao kwa Tume
hii ya Kipapa.
Taarifa inasema, wajumbe wamejadiliana kulingana na maombi yaliyotolewa
na Baba Mtakatifu Francisko, kuhusu umuhimu na malengo ya Tume hii pamoja na kuwashirikisha
watu wengine ili kuweza kuchangia utaalam wao. Wajumbe wamejadili jinsi ambavyo wanaweza
kushirikiana na wataalam mbali mbali katika kulinda na kuwatetea watoto dhidi ya nyanyaso
za kijinsia pamoja na kushirikiana na viongozi mbali mbali kutoka Sekretarieti ya
Vatican. Matunda ya kazi hii yatawasilishwa kwa Baba Mtakatifu kwa ajili ya maamuzi
zaidi.
Tume inapenda kuwahamasisha viongozi wa Makanisa mahalia kuibua mbinu
mkakati utakaosaidia kuwalinda watoto wadogo kwa kwa kukazia: majiundo makini, elimu
na jinsi ya kudhibiti nyanyaso za kijinsia. Kanisa linapenda kuwajibika kikamilifu
katika kuzuia nyanyaso za kijinsia pamoja na kuwahudumia wahanga wa vitendo hivi pamoja
na familia zao.
Kanisa kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, linapenda
kuhakikisha usalama wa watoto dhidi ya nyanyaso. Wajumbe wanaomba sala katika utekelezaji
wa majukumu yao kwa sasa na kwa siku za usoni.