2014-05-03 15:58:37

Vijana jifunzeni kubaki na Yesu, kutembea na kufurahia maisha!


Watu wapya katika Kristo, washiriki wa furaha katika maisha, ndiyo kauli mbiu iliyoongoza mkutano wa kumi na tano wa Chama cha Vijana Wakatoliki Italia, uliofunguliwa hapo tarehe 30 Aprili 2014 na baadaye wakakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, Jumamosi, tarehe 3 Mei 2014. Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi wa Kanisa nchini Italia kwa majitoleo yao katika maisha na utume wa vijana.

Baba Mtakatifu anasema, kauli mbiu ya mkutano mkuu wa Chama cha Vijana Wakatoliki unaeleweka vyema hasa katika kipindi hiki cha Pasaka, Mama Kanisa anpoendelea kutafakari Fumbo la Pasaka, kwa kuangalia jinsi ambavyo wafuasi wa Yesu walivyokutana na Kristo Mfufuka, wakashikwa na furaha kubwa, ambayo waliimwilisha katika undani wao, wakawa na ujasiri wa kutoka kifua mbele kwenda kushiriki mchakato wa Uinjilishaji kwa njia ya ushuhhuda wa maisha.

Baba Mtakatifu anasema, katika mazingira ya wakati huu nchini Italia, vijana wakatoliki wanahimizwa kujikita katika mchakato wa maisha ya kimissionari, kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza ili kutekeleza utume unaojipambanua katika ujana wa maisha ya Kanisa; husan Parokia zile ambazo zinaonekana kuchoka na kujikuta kwamba, zinafungwa.

Parokia kama hizi zinahitaji ari na mwamko wa vijana wanaoshiriki katika huduma inayojikita katika kipaji cha ugunduzi, kwa kuwa na mwelekeo wa kimissionari unaopania kuwafikia watu wote mahali walipo, lakini kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mchakato wa kumfungulia mlango Kristo, ili aweze kwenda nje kukutana na watu. Huu ni uinjilishaji unaopaswa kujikita katika uhalisia wa maisha ya waamini, lakini kwa namna ya pekee miongoni mwa vijana wakatoliki wanaoshikamana na kushirikiana na viongozi wao wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, chama cha vijana wakatoliki Italia ni maarufu sana kwani kimekuwa mstari wa mbele kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, hali inayochangia kuleta mabadiliko katika jamii kwa kujielekeza katika kutafuta mafao ya wengi. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amekazia mambo makuu matatu:

Jambo la kwanza muhimu ni kubaki wakiwa wameshikamana na Yesu, ili kufurahia uwepo wake endelevu kati yao pamoja na kushiriki katika azma ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo, kwani Yeye ndiye chemchemi ya maisha na furaha ya waamini na kwamba, ushuhuda unaotolewa na wakristo unapata maana na mwelekeo mpya kutokana na nguvu mpya inayobubujika kutoka kwa Kristo.

Jambo la Pili anasema Baba Mtakatifu ni kwenda kwenye barabara na viunga vya miji na maeneo yao ili kutangaza kwamba, Mungu ni Baba aliyefunuliwa kwa njia ya Yesu na kwamba, maisha yao sasa yanapaswa kubadilika kwa kuishi kama ndugu wakiwa na matumaini yasiyodanganya kamwe. Wawe na ari na moyo wa kutaka kutangaza Neno la Mungu kwa kukutana na watu mbali mbali; pale wanapoteseka na kutumainia; pale wanapopenda na kuamini; pale ambapo kuna ndoto ya ndani, maswali ya kina na matamanio ya moyo. Hapo anasema Baba Mtakatifu Yesu anawasubiri!

Jambo la tatu ni kufurahia kwa kumshangilia Yesu, kwa kushuhudia zawadi ya maisha, imani sanjari na kutambua karama na mapungufu ya mtu binafsi; mtu mwenye mpango mzuri katika maisha anayetambua kwamba, hata katika giza na utupu wa ndani, kuna dalili za uwepo wa Kristo. Wanapaswa kufurahia kwani wanashirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo na kwamba, wako pamoja na Kristo anayewasindikiza, Maaskofu na Mapadre bila kusahau Parokia na Majimbo yao yanayoendelea kuwatia moyo katika kushiriki hija hii ya maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu anasema, kwa kukazia mambo haya matatu, vijana wanaweza kwenda nje ya mipaka yao kwa kuishi ile furaha ya kuwa ni sehemu ya Wakristo, kwa kuwashirikisha wengine wito wao, hivyo kuepuka vishawishi kwa kuendelea kubaki ndani ya Kristo, kwa kuwashirikisha wengine furaha ya Injili. Anawaombea ili waweze kuona vyema, kusikiliza kwa makini na kuhudumia na kukumbatia. Vijana wawezeshwe kuwa na moyo wa huruma, unaotamani mafao na wokovu wa wote.







All the contents on this site are copyrighted ©.