2014-05-03 16:03:49

Siku ya 90 ya Chuo kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu


Kwa kufuata mafundisho na mfano wa Yesu Kristo, Mwalimu, Kanisa limeendelea daima kutafuta maana ya maisha na ukweli ili kumwilisha utimilifu wake katika maisha ya vijana. Ni katika undani wa maisha ya Kanisa, vyuo vingi vya kikatoliki vimeanzishwa na vinaendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya jamii na Kanisa katika ujumla wake. RealAudioMP3

Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, kilichoanzishwa na Padre Agostino Gemelli pamoja na wasaidizi wake wa karibu, kimekuwa ni msaada mkubwa katika kutoa mafunzo ya kisayansi pamoja na kuendelea kuwa waaminifu kwa mafundisho ya Kanisa, kiasi kwamba, Chuo kikuu hiki kimekuwa ni kimbilio la vijana na matumaini ya wazazi na walezi kwa watoto wao, kwani wana uhakika kwamba, vijana wao watapata majiundo kamili ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Hii inatokana na ukweli kwamba, juhudi hizi zimewashirikisha waamini kwa kuanzisha Siku ya Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambacho kwa Mwaka 2014 kinaadhimisha Siku ya 90, tangu kuanzishwa kwake. Huu ni ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko ulioandikwa na Kardinali Pietro Parolin katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Kardinali Angelo Scola, Rais wa Taasisi ya elimu ya juu ya Giuseppe Toniolo ambayo kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu "pamoja na vijana wahusika wakuu kwa siku za usoni".

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwatia moyo wadau mbali mbali katika Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili kuendeleza Taasisi ya elimu ya juu ya Giuseppe Toniolo, kama njia ya kushuhudia mchango wa Kanisa katika mchakato wa kuwafunda vijana wa kizazi kipya, ili kuendelea kupambana na changamoto za maisha kwa ujasiri mkubwa, hasa katika nyakati hizi ambamo kuna mabadiliko makubwa ya kijamii yanayohitaji majadiliano, ujasiri na uaminifu ili kuendeleza utambulisho wa Kikatoliki katika jamii yenye mwingiliano mkubwa wa kitamaduni.

Baba Mtakatifu anashukuru Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, kitivo cha tiba na upasuaji, kilichoko Hospitali ya Gemelli kwa huduma iliyotukuka ambayo imetolewa na kitivo hiki kwa takribani miaka hamsini iliyopita, kwa wagonjwa na kwamba, katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko ameahidi kutembelea Hospitali ili kukutana na wagonjwa pamoja na wafanyakazi.







All the contents on this site are copyrighted ©.