2014-05-03 15:54:22

Kanisa halina budi kujielekeza katika majadiliano ya kidini, ushuhuda na huduma makini!


Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru Maaskofu kutoka Sri Lanka wanaofanya hija ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano mjini Vatican. Anakumbuka siku ile alipokutana na waamini kutoka Sri Lanka katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 75 ya Sri Lanka kuwekwa chini ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Maaskofu hao wanaendelea kuimarishwa katika imani wakati huu wa hija yao ya kitume.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekiri kabisa utajiri mkubwa wa imani uliofumbatwa wakati wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kwani hii ni zawadi ambayo kamwe hawawezi kupokonywa na mtu yoyote yule. Wanaalikwa na kutumwa kwenda ulimwenguni kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa ujasiri, imani na matumaini na kwa namna ya pekee nchini Sri Lanka ambayo kwa miaka mingi imeshuhudia vita na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwamba, kwa sasa vita imekoma, sasa wabapaswa kujikita katika mchakato wa upatanisho na ujenzi wa taifa la Sri Lanka kama walivyokazia Maaskofu wenyewe katika barua yao ya kichungaji. Kuna haja ya kujikita na kudumisha misingi ya upatanisho, haki msingi za binadamu kwa kuondokana na kinzani za kikabila ambazo bado zinaendelea nchini humo. Baba Mtakatifu anachukua fursa hii kuwafariji wote walioguswa na maafa wakati wa vita na sasa hawana budi kujiimarisha katika imani, kwa wote wanaoendelea kuonja madhara ya vita na kinzani za kikabila.

Kanisa Katoliki nchini Sri Lanka linataka kujielekeza katika mchakato wa upatanisho na ujenzi wa nchi na umoja wa kitaifa, kwa kuponya madonda ya kinzani na utengano wa kikabila, ili kuimarisha umoja na mshikamano unaojikita katika huduma makini katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linapaswa kutambua mambo yale yanayosababisha kinzani kati ya makabila ili liweze kuyapatia ufumbuzi wa kudumu kwa kukazia majadiliano, haki na usawa.

Baba Mtakatifu amelishukuru na kulipongeza Kanisa Katoliki nchini Sri Lanka kwa kuwahudumia waathirika wa Tsunami pamoja na kuendelea kutoa huduma makini katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya wengi kama kielelezo cha ushuhuda wa kinabii katika kuwafariji wote wanaoteseka na kusahauliwa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uvunjifu wa haki msingi za binadamu.

Sri Lanka ni nchi ambayo imekirimiwa utajiri mkubwa wa makabila na waamini wa dini mbali mbali, changamoto kwa Kanisa kujielekeza katika majadiliano ya kidini na majiundo yatakayosaidia kukuza na kudumisha haki na amani, kwa kuwajengea uwezo waamini kuwa kweli ni mashahidi wa imani yao. Misimamo mikali ya kidini na utaifa ni mambo ambayo yanahitaji mikakati makini ya majadiliano ya kidini na Kanisa kuendelea kuwaimarisha waamini wake katika imani sanjari na kukuza Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, shule ya tafakari ya Neno la Mungu na Ibada zinazowawezesha waamini kuwa karibu zaidi na Kristo pamoja na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anasema, Maaskofu hawana budi kuendelea kupandikiza imani na kukoleza upatanisho na majadiliano ya kidini kwa kusaidiwa na Mapadre wao. Wito wa maisha ya kipadre unaendeea kuchanua vyema nchini Sri Lanka na kwamba, wamekuwa kweli ni mfano wa kuigwa katika huduma. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Makleri wanapata majiundo makini: kiakili, kiutu, kiroho na katika mikakati ya shughuli za kichungaji ndani na nje ya Seminari.

Maaskofu waoneshe moyo wa kibaba kwa kuwasaidia kupambana na changamoto za maisha ya Kipadre, ili waendelee kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kujikita katika utakatifu wa maisha kwa sala na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu anawashukuru watawa kutokana na huduma yao kwa watu wa Mungu nchini Sri Lanka hasa katika sekta ya elimu, afya, katekesi na maendeleo vijijini. Ni jukumu la Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawapongeza Maaskofu Katoliki Sri Lanka kwa kukuza na kudumisha utume wa familia kwani familia ni kitovu cha maisha ya kijamii, mahali ambapo wazazi na walezi wanarithisha imani kwa watoto wao. Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Familia itakuwa ni fursa kwa Mama Kanisa kutafuta mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia. Baba Mtakatifu anasema familia zinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira au wakati mwingine kutengana na wapendwa wao kwa kutafuta kazi.

Kuna ongezeko kubwa la ndoa mchanganyiko, jambo linalohitaji mikakati ya kichungaji kwa ajili ya kuwasaidia watoto kukua na kukomaa katika imani, ili kushuhudia nakuwafunda watoto katika imani. Kumbe, kuna haja ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya familia.







All the contents on this site are copyrighted ©.