2014-05-03 16:33:44

Jifungeni kibwebwe kukabiliana na upungufu wa madawati Tanzania


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema shule za msingi hapa nchini zinakabiliwa na upungufu wa madawati karibu milioni moja na nusu ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ijifunge mkanda na kulipa kipaumbele suala la kupunguza tatizo hilo.
Ametoa agizo hilo Jumamosi, Mei 3, 2014 wakati akiwahutubia mamia ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma ambao walihudhuria uzinduzi wa Wiki ya Elimu Tanzania kwenye uwanja wa Jamhuri.
“Takwimu nilizonazo zinaonyesha kuwa Tanzania ina mahitaji ya madawati 3,302,678 wakati madawati yaliyopo ni 1,837,783 kwa hiyo tuna upungufu wa madawati 1,464,895 katika shule zetu za msingi,” alisema Waziri Mkuu.

Kutokana na mahitaji hayo, Waziri Mkuu alisema endapo Serikali itaamua kutengeneza madawati 100,000 kwa mwaka kwa gharama ya sh. bilioni 12/-, itachukua miaka 15 kumaliza tatizo hilo ili kuziba pengo lililopo sasa.
“Nimepita kwenye banda la Taasisi ya Maajar Trustna pale wameniambia kuwa wameshatengeneza madawati 12,000 na kuyagawa katika mikoa sita. Wastani wa kila dawati ni sh. 120,000/- lakini inategemea na upatikanaji wa mbao pamoja na gharama za ufundi.”
“Tukichukua gharama zao, tukaamua kutengeneza madawati 200,000 kwa mwaka, itatugharimu sh. bilioni 24 na itachukua miaka saba kumaliza tatizo hilo wakati tukiamua kutengeneza madawati 300,000 kwa mwaka, itatugharimu sh. bilioni 36 na itachukua miaka mitano kumaliza tatizo hilo,” alifafanua Waziri Mkuu.
Alisema ni lazima hatua madhubuti zichukuliwe kumaliza tatizo hilo kwani inatia aibu na hakuna sababu ya kuendelea kuona wanafunzi wakisoma huku wamekaa chini.
“Waziri wa Elimu na watu wako ni lazima mjifunge mkanda na kipaumbele chenu kiwe ni kupunguza tatizo la madawati katika muda mfupi sana; na itakuwa vema kama mtajipanga haraka ili mje na suluhisho ndani ya wiki hii kabla Mheshimiwa Rais hajaja kufunga maonyesho haya,” aliongeza.
"Kaeni na watu wa Taasisi ya Maajar Trustmuone ni kwa njia gani mnaweza kutatua tatizo hili… kama ni kuandaa chakula cha hisani ili kuchangia madawati fanyeni hivyo ili tatizo hili liishe. Wako Watanzania wanaweza kuchangia dawati moja, mawili, matatu au zaidi na tukajikuta tumemaliza tatizo hili,” alisema.
“Na ninyi wa TAMISEMI kaeni na kuandaa utaratibu wa kuondoa tatizo hili. Kila Halmashauri kwa nafasi yake iwe ya mjini au ya vijijini ina uwezo wa kupunguza tatizo kulingana na fursa ilizonazo. Nasisitiza jambo hili liwe ni ajenda ya kudumu,” aliongeza.
Wakati huohuo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Idris Kikula, akitoa shukrani kwa niaba ya wadau wa elimu alisema anaunga mkono hoja ya uchangiaji wa madawati na kusisitiza kuwa kuna haja ya watu kubadili mtazamo walionao kuhusu suala la uchangiaji wa huduma za kijamii.
“Kuna watu ukiwaambia kuchangia madawati wanakataa lakini wako waliopokea kadi nyingi za michango ya harusi na wako tayari kuzichangia kwa sababu wanajua huko kuna kula na kunywa. Niwasihi wananchi tubadilishe mtazamo wetu na tuisaidie Serikali katika suala hili la madawati kwa watoto wetu,” alisema.








All the contents on this site are copyrighted ©.