2014-05-03 07:22:10

Jengeni na kudumisha mchakato wa urafiki na majadiliano ya kidini!


Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza Wakristo nchini Algeria kuwa ni kielelezo cha Kanisa ambalo liko wazi kwa ajili ya kujenga na kudumisha mchakato wa urafiki na majadiliano ya kidini, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu yuko karibu na waamini wa Kanisa Katoliki nchini Algeria katika maisha na utume wao kwa kutambua kwamba, wanaishi katika nchi ambayo ina idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam. RealAudioMP3

Hayo yamesemwa na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini katika Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya Miaka mia moja tangu Kanisa la Mtakatifu Augustino lilipopewa hadhi ya kuwa Kanisa kuu, katika Jimbo Katoliki la Costantina, nchini Algeria, tarehe 2 Mei 2014.

Katika mahubiri yake, Kardinali Tauran anasema, Kanisa kuu lililojengwa nje ya Roma ni kielelezo cha umoja na mshikamano na Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, lililoko mjini Vatican. Ni Kanisa ambalo linapaswa kuwa na Mtakatifu msimamizi ambaye, waamini wanapaswa kufuata na kuiga mfano wa utakatifu wa maisha yake.

Ndiyo maana, waamini wanachangamotishwa na Kanisa kuiga mfano wa Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, aliyejitosa kimasomaso kufundisha ukweli kwa kumwangalia mtu kutoka katika undani wa maisha yake. Ni Mtakatifu anayeendelea kukazia umuhimu wa kujenga na kuimarisha: upendo ili kukuza haki na amani; kugundua na kutambua uwepo wa Mungu kutoka katika undani wa maisha ya kila mtu, katika uzuri wa mazingira na mawazo angavu yanayojikita katika urafiki na mwingiliano wa watu!

Kanisa kuu la Mtakatifu Augustino lililokarabatiwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita bado linaonesha mawazo na mafundisho makuu ya Mtakatifu Augustino kama mawe hai yanayopaswa kujenga na kuiimarisha Jumuiya ya Wakatoliki, kwa kuendeleza uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake; majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam pamoja na kushirikiana na wote katika kutafuta mafao na ustawi wa wananchi wote wa Algeria.

Kanisa kuu la Mtakatifu Augustino, liwe ni kielelezo chenye mvuto na mashiko kwa watu wenye kiu ya kutaka kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao, ili waweze kupata mahali nyumba ambamo wanaweza kusali katika mchakato wa kutafuta ukweli, upendo na uhuru, tema ambazo ni msingi katika mafundisho ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa.

Kardinali Tauran anasema, Mtakatifu Augustino alipambana kwa ujasiri mkubwa na changamoto zilizojitokeza wakati wa uhai wake, kama ilivyo kwa wakati huu ambapo kuna mabadiliko makubwa ya kitamaduni na kisiasa, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuyaangalia yote haya kwa jicho la moyo, kwa kusikiliza kilio cha binadamu katika ulimwengu mamboleo!

Hawa ni watu wasiokuwa na fursa za ajira; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha; ni watu waliosahaulika, wafungwa na wote wanaoteseka! watu hawa waguswe na utakatifu pamoja na hekima ya Mtakatifu Augustino.







All the contents on this site are copyrighted ©.