2014-05-02 08:24:12

Watoto wengi wanaendelea kufariki dunia kutokana na ukosefu wa dawa


Ukosefu wa dawa muhimu kwa ajili ya watoto wadogo ni janga ambalo linawaandama watoto wanaozaliwa na kuishi katika Nchi changa zaidi duniani. Hata kile kiasi kidogo cha dawa kinachozalishwa kinashindwa kuwafikia walengwa mahali waliko na kwa wakati muafaka.

Hii ni sehemu ya taarifa iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani, linalobainisha kwamba, walau kuna zaidi ya watoto millioni tisa wenye umri chini ya miaka mitano wanafariki dunia kutokana na magonjwa ambayo yangeweza kutibiwa kwa dawa zenye ufanisi na madhubuti.

Shirika la Afya Duniani linasema kwamba, vifo hivi ni kutokana na ukweli kwamba, dawa nyingi hazijatengenezwa kwa ajili ya kukidhi tiba na mahitaji ya watoto wagonjwa kwa kuzingatia uzito, umri na hali ya mtoto mgonjwa. Dawa hizi ni zile zinazotibu ugonjwa wa Malaria, Ukimwi na Kifua kikuu. Inakadiriwa kwamba, kiasi cha watoto millioni tatu wenye umri chini ya miaka mitano wanafariki kila mwaka kutokana na magonjwa ya kuhara, ingawa kuna dawa ambazo zingeweza kudhibiti magonjwa haya. Lakini kwa bahati mbaya dawa hizi ambazo ni dawa msingi wakati mwingine zinakosekana kabisa katika maduka ya dawa na Hospitali.

Wataalam wa Shirika la Afya Duniani wanakiri kwamba, wakati mwingine watoto hupewa dawa zilizokusudia kutibu magonjwa ya watu wazima kwa kuzimega, jambo ambalo wakati mwingine si rahisi sana kwa wazazi na walezi, kwani hapa kuna hatari ya watoto kuzidishiwa kipimo cha dawa au kupata pungufu ya kipimo kilichokuwa kinakusudiwa!







All the contents on this site are copyrighted ©.