Baraza la Makanisa Zambia, CCZ hivi karibuni katika taarifa yake kwa vyombo vya habari
linasema kwamba, limesikitishwa na vitisho vilivyotolewa na Rais Michael Chilufya
Sata wa Zambia dhidi ya Askofu George Lungu wa Jimbo Katoliki Chipata, baada ya kusali
Jimboni kwake kwa ajili ya kuiombea Serikali ya Zambia iweze kuwapatia wananchi Katiba
mpya.
Baraza la Makanisa Zambia linasema, vistisho hivi haviwezi kukubalika
kamwe, kwani wananchi wa Zambia wanahitaji Katiba Mpya ambayo imekuwa ikipigwa dana
dana na viongozi mbali mbali wa Serikali wanapoingia madarakani. Baraza la Makanisa
linasema katika taarifa yake kwamba, Makanisa hayawezi kukaa kimya na kuwaona wananchi
wa Zambia wakiendelea kuogelea katika umaskini, ujinga na maradhi, huku watu wachache
wakiendelea kufaidika na rasilimali za nchi kutokana na ukosefu wa wa utawala bora.
Katiba
Mpya nchini Zambia ni hitaji msingi na kamwe Makanisa hayatakaa kimya, hadi pale wale
waliopewa dhamana na madaraka ya kuwaongoza wananchi wa Zambia watakapotekeleza wajibu
wao na kwamba, kuomba Katiba Mpya si kwamba Kanisa linataka kuingilia mambo ya kisiasa,
bali linatekeleza sauti yake ya kinabii kwa wananchi wasiokuwa na sauti! Watu ambao
wanataka kunyamazishwa na wenye madaraka serikalini.
Baraza la Makanisa Zambia
linamwomba, Rais Michael Sata kuwapatia wananchi wa Zambia Katiba Mpya bila kuchelewa
kabla mambo hayajaharibika.