2014-05-02 09:34:50

Uwajibikaji wa binadamu katika kudumisha mazingira endelevu!


Taasisi ya Kipapa ya Sayansi kwa kushirikiana na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 6 Mei, 2014, zinaendesha Warsha ya pamoja inayojadili pamoja na mambo mengine kuhusu binadamu anavyoendeleza utunzaji wa mazingira asilia kwa ajili ya mafao yake kwa sasa na kwa vizazi vijavyo; kwa kuibua na kubuni mikakati na sera za uchumi endelevu; pamoja na matumizi sahihi ya ujuzi na maarifa.

Hii inatokana na ukweli kwamba, mwanadamu anahitaji mazingira bora kwa ajili ya ustawi na maendeleo yake, lakini takwimu zinaonesha kwamba, mwanadamu amekuwa pia ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira kutokana na matumizi mabaya ya rasilimali ardhi. Binadamu anapaswa kubadili tabia na mwenendo wake wa maisha. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la mahitaji ya chakula duniani, watu wanaishi kwa muda mrefu zaidi na hali ya uchumi kwa mataifa mengi imeboreka kwa kiasi kikubwa, lakini tatizo la uharibifu mkubwa wa mazingira kwa sasa na kwa siku za usoni kati ya changamoto kubwa ambazo Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuzikabilia.

Kuna baadhi ya watu wanahusisha ukuaji wa uchumi na uchafuzi wa mazingira na kwamba, baadhi ya wataalam wanapenda kugusia suala la mikakati ya maendeleo endelevu, wanapozungumzia ukuaji wa uchumi kimataifa, pengine na kusahau kuangalia changamoto za ukuaji wa uchumi katika nchi zinazoendelea duniani. Lakini ikumbukwe kwamba, uchafuzi wa mazingira unaosababisha athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi ni chanzo kikubwa cha majanga kwa nchi tajiri na maskini duniani.

Kukua na kukomaa kwa uchumi katika nchi tajiri katika sekta ya viwanda na kilimo, kumechangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira duniani na kwamba, hadi sasa hakuna sera makini zilizokwisha ibuliwa ili kudhibiti hali kama hii, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Brazil, Russia, India, China na Afrika ya Kusini, BRICS kama zinavyotambuliwa na wengi zinaendelea kufuata mkondo huo huo wa uchafuzi wa mazingira kiasi cha kuhatarisha maisha ya viumbe hai kwa siku za usoni.

Takwimu zinaonesha kwamba, idadi ya watu duniani inaendelea kuongezeka maradufu, kiasi kwamba hata mahitaji ya nishati yanaongeza kwa kasi ya ajabu; mambo yote haya yanachangia kwa kiasi kikubwa uharibu wa mazingira. Kupanuka kwa kiwango cha elimu na ufahamu wa masuala ya kisayansi, uwekezaji katika miundo mbinu, ubora wa elimu ya juu na ukuaji wa viwanda ni kielelezo kwamba watu wengi wamekuwa na ufahamu mkubwa wa madhara ya uchafuzi wa mazingira katika Nchi tajiri zaidi duniani ikilinganishwa na watu wanaoishi katika nchi maskini.

Taasisi za Kipapa za Sayansi na Sayansi Jamii zinasema kwamba, dhamana na uwajibikaji wa kimaadili ni muhimu sana, ingawa ni jambo ambalo halijapewa msukumo wa kutosha. Kuna haja ya kufanya mabadiliko yanayolenga kuleta maboresho katika uhusiano kati ya binadamu na mazingira, ili kuibua na kuimarisha mikakati itakayosaidia kuendeleza sera na mipango endelevu ya kiuchumi na maendeleo jamii.

Mkutano wa Kimataifa katika kudhibiti madhara ya mabadiliko ya tabianchi uliofanyika mjini Rio de Janairo, ulishindwa kufikia malengo yake kutokana na misigano mikubwa iliyojionesha kati ya wajumbe waliokuwa wanahudhuria. Wajumbe wa Taasisi za Kipapa za Sayansi na Sayansi Jamii zinataka kuhimiza ubinadamu endelevu kwa ajili ya kuenzi mazingira bora, kwa kutambua kwamba, mwanadamu na mazingira ni mambo yanayotegemeana katika: mahitaji, chakula, afya na nishati. Watalaam kutoka katika medani za sayansi na sayansi jamii wakishirikiana kwa dhati wanaweza kuleta uhusiano mwema kati ya binadamu na mazingira yake.







All the contents on this site are copyrighted ©.