2014-05-02 14:23:09

Rais Dos Santos wa Angola akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 2 Mei 2014 amekutana na kuzungumza na Rais Josè Eduardo dos Santos wa angola pamoja na ujumbe wake, ambaye baadaye amekutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Viongozi hawa wawili wamepongeza uhusiano mwema kati ya nchi hizi mbili, hasa zaidi kwa serikali ya Angola kulitambua kisheria Kanisa Katoliki. Kwa pamoja wamekiri mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Angola hususan katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya watu.

Wamegusia changamoto za kitaifa, kikanda na kimataifa zinazoendelea kujitokeza sanjari na mapambano dhidi umaskini, ukosefu wa usawa kijamii; maendeleo endelevu ya binadamu, upatanisho, haki na amani bila kusahau vita inayoendelea sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.