2014-05-02 12:00:38

Papa atokwa machozi kutona na mauaji ya Wakristo!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican Ijumaa tatehe 2 Mei 2014 anasema, amelia kwa uchungu mkubwa kusikia habari za Wakristo wanaoendelea kuuwawa, kudhulumiwa na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hivi ni vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watu wenye misimamo mikali ya kiimani, wanaodhani kwamba, wanatekeleza mapenzi ya Mungu kwa njia hii.

Akizungumzia kuhusu Injili inayomwonesha Yesu akifanya muujiza wa kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, anasema, kuna haja ya kukazia mambo makuu matatu: upendo unaoneshwa na Yesu kwa watu wake; Yesu anaguswa na matatizo pamoja na mahangaiko ya watu na kwamba, wafuasi wake hawana sababu ya kuogopa, kwani Kanisa litaendelea kustawi na kuchipua kama mtende wa Lebanoni; litatangaza Injili na kwamba, Yesu yuko pamoja na wafuasi wake akizungumza kwa njia ya nguvu ya upendo.

Baba Mtakatifu anasema, wivu ni mwendelezo wa kazi ya shetani, lakini haukuwazuia watu kumfuasa Yesu, licha ya kwamba walikumbana na nyanyaso pamoja na madhulumu kutoka kwa Wakuu wa Makuhani na Mafarisayo. Wivu uliwapelekea hata kutoa rushwa ili kuunyamazisha ukweli kuhusu ufufuko wa Yesu Kristo, ili kuwapotosha watu wasiuone mwanga na ukweli juu ya Yesu Kristo Mfufuka.

Baba Mtakatifu anasema, ni Gamalieli mwalimu wa torati, mtu mwenye haki na kuheshimiwa na wengi aliyewaonya Wakuu wa Makuhani na wao wakabadili mwelekeo wao na hivyo kumwachia Yesu nafasi ya kukutana na watu kwa njia ya Mitume wake. Viongozi hao waliwacharaza viboko mitume na kuwaachia kuendelea na kazi ya kutangaza Injili.

Hata leo hii kuna baadhi ya viongozi wa dunia hii wanaoendeleza nyanyaso na madhulumu dhidi ya Wakristo, jambo la msingi ni kuona kwamba, hata katika madhulumu haya yote, bado kuna Wakristo wenye ujasiri na wanaendelea kutoa ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.