Michezo ipewe hadhi na heshima yake kama chemchemi ya furaha, majiundo na ukomavu
wa mtu!
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 2 mei 2014 amekutana na kuzungumza na Timu
ya Mpira ya Fiorentina na Napoli walioingia fainali ya Kombe la Italia pamoja na viongozi
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Italia. Amewashukuru kwa kutambua dhamana na wajibu
wao wa kijamii, kwani mpira wa miguu unawawajibisha wachezaji ndani na nje ya uwanja
kama ilivyo kwa viongozi wa timu za mpira wa miguu katika ngazi mbali mbali.
Baba
Mtakatifu amewakumbusha kwamba, alipokuwa kijana alipendelea sana kwenda kuangalia
mpira wa miguu huku akiwa ameambatana na ndugu zake siku za jumapili, kwani haya yalikuwa
ni matukio ya furaha, changamoto na mwaliko wa kufanya michezo iwe ni chemchemi ya
furaha. Mchezo wa mpira wa miguu ni kitega uchumi kikubwa kwa wafanyabiashara wanaopeleka
matangazo yao ya biashara na kwa vituo vya televisheni kama chanzo cha mapato.
Baba
Mtakatifu Francisko anaonya kwamba, mwelekeo wa uchumi usipewe kipaumbele cha kwanza
katika michezo kwani kitachafua mambo mengine katika ngazi mbali mbali. Michezo haina
budi kupewa hadhi na heshima yake kwa kuhakikisha kwamba, wachezaji wanawajibika barabara,
kwani wanatazamwa watu wengi, lakini sehemu kubwa ya mashabiki wao ni vijana, mwaliko
wa kuwa na nidhamu na adabu njema kama wana michezo bora.
Baba Mtakatifu katika
hotuba yake kwa wanamichezo na viongozi hawa anawakumbusha kwamba, michezo ina dhamana
ya pekee katika elimu, malezi na ukomavu wa mtu kiroho, kimwili na kijamii; kwa kujenga
na kuimarisha mshikamano, katika ukweli na heshima. Haya ndiyo mambo msingi ambayo
mpira wa miguu unapaswa kuyaendeleza.