Askofu mteule Moses Hamungole wa Jimbo Katoliki Monze, Zambia aliyeteuliwa hivi karibuni
na Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwekwa wakfu na hatimaye kusimikwa kuwa Askofu
Monze, Jumamosi tarehe 3 Mei 2014.
Padre Chrisantus
Ndaga, Katibu wa Idara ya habari, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika
Mashariki na Kati, AMECEA anasema kwamba, Askofu mteule Moses ni fahari ya Idara ya
habari ya AMECEA kwani anakuwa ni Askofu wa tatu katika orodha ya Maaskofu waliowahi
kuteuliwa kutoka Idara hii. Wa kwanza alikuwa ni Askofu Joseph Mkwaya na Askofu Fortunatus
Lukanima; Maaskofu wote wawili wamekwisha kufariki dunia.
Padre Ndaga anasema,
katika Ibada ya Misa Takatifu ya kuwekwa wakfu na hatimaye kusimikwa, ujumbe wa AMECEA
unapenda kushiriki kikamilifu kwa njia ya uwepo na mshikamano wa sala, wakati huu
Askofu Mteule Moses Hamungole anapopewa utume wa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza
watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Monze, Zambia. AMECEA itaendelea kushirikiana na na
Jimbo Katoliki Monze kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Monze na AMECEA katika ujumla
wake.