Mkutano wa Makardinai washauri wakuu wa Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa
mageuzi makubwa ndani ya Kanisa Katoliki umehitimishwa mjini Vatican siku ya Jumatano,
tarehe 30 Aprili 2014. Mkutano huu umemaliza kimsingi kufanya tathmini na upembuzi
wa kina kuhusu Mabaraza na Halmashauri za Kipapa.
Kardinali Lorenzo Baldisseri,
Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, amewasilisha taarifa kuhusu mchakato wa maadhimisho
ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, itakayoadhimishwa Mjini Vatican,
Mwezi Oktoba, 2014. Makardinali washauri wataendelea tena na kazi yao, mwanzoni mwa
Mwezi Julai, 2014.
Ijumaa tarehe 2 Mei, 2014 kwa mara ya kwanza Baraza la Kipapa
la Uchumi lililoanzishwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko, litafanya kikao
chake mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutoa hotuba elekezi wakati
wa ufunguzi wa Baraza hili jipya. Ajenda kuu ya mkutano huu ni kuandika Katiba ya
Baraza na ratiba elekezi ya kazi zitakazofanywa na Baraza hili, ili kuleta ufanisi
na tija katika masuala ya uchumi mjini Vatican. Mkutano huu utafanyika kwa siku nzima
ya Ijumaa.
Wakati huo huo, kuanzia Mei Mosi hadi tarehe 3 Mei, 2014 Tume ya
Kipapa kwa ajili ya kulinda watoto inaanza mkutano wake wa kwanza tangu ilipoundwa
na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni. Wajumbe wanazungumzia kuhusu asili na malengo
ya Tume hii pamoja na kuangalia uwezekano wa kuwashirikisha wajumbe wengine kutoka
sehemu mbali mbali za dunia.