Fedha ikithaminiwa sana, uwepo wa Mungu na utu wa mwanadamu vinawekwa rehani!
Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani
kwa mwaka 2014 linasema kwamba, pale jamii inaposhindwa kutoa kipaumbele cha kwanza
kwa utu na heshima ya binadamu pamoja na uwepo wa Mungu na badala yake fedha na mali
vinapewa msukumo wa pekee, hapo kuna hatari ya kuibuka kwa misigano ndani ya Jamii
na hivyo kukwamisha mchakato wa maendeleo endelevu unaogusa mahitaji ya mtu kiroho
na kimwili.
Maaskofu wanaendelea kusema kwamba, pale fursa za ajira zinapokosekana,
utu na heshima ya mwanadamu vinawekwa rehani. Ukosefu wa fursa za ajira, mazingira
duni ya kazi, athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kazi za suluba zinazofanywa na
watoto, ubaguzi wa rangi na ukosefu wa usawa katika utoaji wa mishahara pamoja na
mazingira mabaya ya kazi ni mambo ambayo yanasababisha madonda makubwa katika utu
na heshima ya wafanyakazi, kiasi kwamba, athari zake pia zinajionesha kwenye familia
kwa kushindwa kutekeleza nyajibu zake barabara.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Hispania linawaalika kwa namna ya pekee waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha
upendo na mshikamano wa dhati na wafanyakazi wanaokumbana na athari za myumbo wa uchumi
kimataifa, kiasi kwamba hawana tena matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi.
Maaskofu
wanawakumbuka wafanyakazi waliopoteza maisha yao wakiwa wanatoa huduma kwa jamii,
matukio ambao kimsingi yanasababishwa na ukosefu wa usalama kazini na maelezo ya kina.
Vifo na ajali kazini ni matukio ambayo yanaacha madonda makubwa kwa familia za wafanyakazi
na taifa katika ujumla wake, kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, usalama kazini
unapewa pia kipaumbele cha kutosha.
Vyama vya wafanyakazi visipotekeleza dhamana
na wajibu wake, wafanyakazi wataendelea kupoteza maisha, kupata vilema vya kudumu
na hatimaye, watatumbukia kwenye umaskini wa hali na kipato!
Maadhimisho ya
Siku ya Wafanyakazi Duniani, iwe ni fursa kwa wafanyakazi kutekeleza wajibu wao kikamilifu
kwa kutambua kwamba, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Kazi ambayo
mtu ameichagua kwa hiyari yake mwenyewe inachangia kwa kiasi kikubwa mchakato wa maendeleo
ya Jamii inayomzunguka; kwa kukidhi mahitaji ya familia pamoja na kuacha chapa ya
kudumu katika maisha ya mtu binafsi, kifamilia na katika maisha ya kiroho.