2014-04-30 11:22:13

Wanawake waandamana Nigeria kupinga vitendo vya Boko Haram


Wanawake na wadau mbali mbali nchini Nigeria, Jumatano tarehe 30 Aprili 2014 wameamua kujitokeza hadharani kupinga vitendo vya mauaji, utekaji nyara na udhalilishaji wa utu na heshima ya binadamu vinavyofanywa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria.

Wanawake hawa wanataka Kikundi cha Boko Haram kuwaachilia mara moja wasichana wa shule ya Chibok waliotekwa nyara hivi karibuni. Maandamano makubwa yameandaliwa na wanawake kutoka Jimbo la Borno, ngome ya Kikundi cha Boko Haram na kuungwa mkono na vyombo vya habari nchini Nigeria.

Wanawake nchini Nigeria wameamua kuweka kando tofauti zao za kiimani, kiitikadi na kikabila ili kuonesha mshikamano wa dhati unaopania kuweka shinikizo zaidi kwa Boko Haram ili kuweze kuwaachia wasichana waliotekwa nyara na wengi wao bado hawajapatikana na wala hawajulikani waliko hadi sasa. Wazazi wanasema bado kuna wasichana 234 ambao wako mikononi mwa Kikundi cha Boko Haram tangu walipotekwa nyara.







All the contents on this site are copyrighted ©.