2014-04-30 14:20:49

Paji la akili liwawezeshe kuona mpango wa Mungu unaojikita katika upendo


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 30 Aprili 2014 ameendelea na Katekesi yake kuhusu Karama za Roho Mtakatifu, kwa kutafakari kuhusu kipaji cha akili. Hii ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu inayomshikirisha mwamini maisha ya Kimungu kwa njia ya Imani inayopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, ili kuweza kuona katika historia mpango wa Mungu wa milele unaojikita katika upendo.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Roho Mtakatifu anaishi katika mioyo ya waamini anaisaidia na kuiongoza akili ili kuweza kufahamu kwa undani zaidi mafundisho ya Yesu na kazi yake ya ukombozi. Kama ilivyokuwa kwa Wafuasi waliokuwa njiani kwenda Emau, wakati mwingine inawawia vigumu wakristo kutambua kwamba, Yesu anatembea pamoja nao na kwamba, kuna neema ya Mungu katika maisha na ulimwengu unaowazunguka.

Baba Mtakatifu Francisko anasema ni kwa njia ya kipaji cha akili kwamba, macho na mioyo ya waamini inaweza kufunguka na kuwaka ndani mwao wanapotambua uwepo wa Yesu Kristo Mfufuka na hivyo kupata fursa ya kuona mambo yote katika mwanga mpya na mwelekeo mpya wa maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kusali ili kumwomba Roho Mtakatifu paji la ufahamu! Kwa njia ya Roho Mtakatifu giza lote linalojikita katika akili na mioyo ya binadamu linaweza kutokomea; kwa kuimarisha imani na hivyo kuwasaidia kuonja utajiri wa Neno la Mungu na ahadi za ukombozi.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoa nafasi kwa kipaji cha akili ili kutambua katika historia na matukio ya maisha mpango wa upendo wa Mungu kwa waja wake; matumaini na amani. Waamini wanaendelea kuchangamotishwa kuwa kweli ni mashahidi wa tunu msingi za maisha ya Kikristo ndani ya Jamii.

Paji la akili anasema Baba Mtakatifu, linawawezesha waamini kulifahamu Fumbo la Utatu Mtakatifu, chemchemi ya imani inayomwilishwa kwa utimilifu wake katika maisha ya kila siku. Anawataka waamini kumwachia Roho Mtakatifu nafasi ili aweze kuwawashia moto wa mapendo na kuwa kweli Wamissionari wa upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko ametambua kwa namna ya pekee uwepo wa kundi kubwa la mahujaji kutoka Poland, ambalo limekuwepo mjini Roma kushuhudia kutangazwa kwa watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo wa Pili.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa waamini kutolea ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo, kwa kujiachilia kwenye huruma ya Mungu, hasa kwa nyakati hizi ili iendelee kustawi katika maisha na nia njema walizo nazo. Waamini wanapofanya hija ya maisha ya kiroho watambue kwamba, wao ni sehemu ya Taifa la Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.