Makardinali washauri wakuu kukamilisha kazi yao mwaka 2015
Mkutano wa Makardinali washauri wakuu wa Papa Francisko katika mchakato wa mageuzi
ndani ya Kanisa kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 Aprili 2014 wamekuwa na vikao ambavyo
vinahudhuriwa pia na Baba Mtakatifu Francisko hapa mjini Vatican kadiri ya nafasi
ya ratiba yake.
Hili ni kundi la Makardinali wanane walioteuliwa na Baba Mtakatifu
Francisko hivi karibuni ili kumshauri katika masuala ya kufanya mabadiliko makubwa
katika Sekretarieti ya Vatican kadiri ya matakwa yaliyooneshwa na Makardinali wakati
wa mikutano yao elekezi kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mikutano
hii pia inahudhuriwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ambaye kimsingi
ndiye mtendaji mkuu katika Sekretarieti ya Vatican.
Hadi sasa Makardinali wamesikiliza
kwa umakini mkubwa taarifa kutoka kwa Joseph F. X. Zahra, Rais wa Tume ya Kipapa inayojishughulisha
na masuala ya uchumi na uongozi mjini Vatican, COSEA, mintarafu sekta ambazo zimechambuliwa
na tume yake.
Makardinali wamepembua kwa kina na mapana Mabaraza ya Kipapa
yanayotekeleza dhamana na utume wake mjini Vatican, kwa sasa wameanza uchambuzi wa
Halmashauri za Kipapa na baadaye watafanya upembuzi wa jumla. Makardinali wataendelea
na kazi yao tena kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 4 Julai 2014.
Taarifa iliyotolewa
na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican inabainisha kwamba, bado kuna
kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Makardinali hawa na pengine, inaweza kukamilika
ifikapo mwaka 2015. Ijumaa tarehe 2 Mei 2014 kutakuwa na mkutano wa kwanza wa Baraza
la Kipapa la Uchumi.