Kazi inayoheshimu utu wa binadamu ni nyenzo msingi katika mapambano dhidi ya umaskini
duniani!
Fursa za ajira na kazi inayoheshimu na kuthamini utu wa mwanadamu ni nyenzo msingi
katika mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani unaongezeka maradufu licha ya maboresho
katika maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na utandawazi.
Hii ndiyo
changamoto inayotolewa na Baraza la Kipapa la haki na amani katika semina ya siku
mbili iliyofunguliwa siku ya Jumanne, tarehe 29 Aprili 2014. Semina hii inahudhuriwa
na wajumbe kutoka Shirika la Kazi Duniani, ILO, Mashirika ya Kanisa Katoliki yanayojihusisha
na masuala ya kazi pamoja na wadau wengine muhimu waliotia sahihi katika Waraka unaokazia
umuhimu wa kuwa na kazi inayoheshimu na kuthamini utu wa mwanadamu kwa ajili ya maendeleo
endelevu mara baada ya mwaka 2015. Dhana hii imejadiliwa kwa kina na mapana katika
siku yake ya kwanza.
Semina hii ya kimataifa inayofanyika mjini Roma imefunguliwa
rasmi na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, kwa kuwashukuru
watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II waliosimama kidete kulinda na kutetea masilahi
ya wafanyakazi, haki na amani; mambo yanayojionesha kwa namna ya pekee katika kukazia
fursa za ajira na kazi ambayo kimsingi ni kielelezo cha ukamilifu, utu na heshima
ya binadamu kama sehemu ya mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi
ya baa la umaskini duniani.
Kardinali Turkson anasema kwa uchungu kwamba, licha
ya maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mchakato wa uzalishaji viwandani sanjari
na utandawazi, lakini umaskini unaendelea kunyanyasa mamillioni ya watu, kwa kusema
katika lugha nyepesi, lakini ukweli ni kwamba, kuna mabillioni ya watu ambao wanaendelea
kuogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato, licha ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa
na binadamu katika karne ya ishirini na moja.
Tafiti mbali mbali zinaonesha
kwamba, kuna ongezeko kubwa la watu wasiokuwa na fursa za ajira, wengine wanafanya
kazi katika mazingira na duni na kwa kiwango cha chini kabisa; mambo ambayo kimsingi
yanachangia kuporomoka kwa heshima na thamani ya kazi kama utimilifu wa utu na heshima
ya binadamu. Pale ambako kuna maboresho makubwa ya fursa za ajira, hapo kuna cheche
za maendeleo kwa wafanyakazi na familia zao; maboresho ya huduma ya elimu na afya;
kimsingi hii ni fursa kubwa katika maendeleo ya jamii husika.
Wajumbe wa semina
hii ya kimataifa wanachambua tema ya kazi si tu kama njia ya kupambana na baa la umaskini
duniani, bali pia wanaangalia fursa za kazi miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, wafanyakazi
wahamiaji pamoja na mkakati wa utunzaji bora wa mazingira. Kuna haja anasema Kardinali
Turkson kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta hali bora na zenye usalama zaidi, ili kukoleza
jitihada za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo hadi sasa yamesababisha majanga
makubwa kwa watu na mali zao.
Wajumbe wa semina wanaongozwa na Mafundisho Jamii
ya Kanisa pamoja na mchango wa Mapapa mbali mbali katika kukuza na kudumisha utu na
heshima ya binadamu; maendeleo ya watu yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho
na kimwili; ukweli katika upendo. Yote haya anasema Kardinali Turkson yanaonesha kwamba,
kazi na maendeleo ya mwanadamu ni sawa na chanda na pete, kamwe hayawezi kutenganishwa,
kwani yanalenga mafao ya wengi. Bila kazi, mafao ya wengi yako mashakani.
Baba
Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kichungaji, Injili ya Furaha anafanya rejea
katika dhana hii, kwa kukazia umuhimu wa elimu makini, huduma bora za afya na kazi
inayojikita katika: uhuru, ubunifu, ushirikishwaji na mshikamano kama kielelezo makini
cha utu na heshima ya binadamu, ulinzi na utetezi wa maisha.
Baba Mtakatifu
anaendelea kuichangamotisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inalinda na kutetea
utu na heshima ya wafanyakazi. Ukosefu wa fursa za ajira ni jambo ambalo linahatarisha
na kugumisha hali ya watu wengi duniani. Kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa, inaonekana
kwamba, ukuaji wa uchumi kwa nchi nyingi umedumaa, hauna tena uwezo wa kujiongeza
na kutengeneza fursa za ajira, kutokana na sababu msingi kwamba, fedha imepewa kipaumbele
cha kwanza, utu na heshima ya binadamu vikawekwa rehani.
Kardinali Peter Turkson
anaendelea kuwahimiza wachumi, watunga sera na wadau mbali mbali kujikita katika mchakato
wa maendeleo ya uchumi yanayosimikwa katika misingi ya haki na mshikamano wa kidugu.
Athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinapaswa kushughulikiwa kwa kina na mapana kwa
kutumia nyenzo za ubunifu, ili kujenga na kuimarisha mifumo mipya ya ushirikiano wa
kimataifa.
Semina hii ya kimataifa inahitimishwa Jumatano tarehe 3o Aprili,
2014 katika mkesha wa Siku kuu ya Wafanyakazi, yaani Mei Mosi, ambayo kwa mwaka huu
inaadhimishwa, huku watu wengi wakiwa bado wameelemewa na athari za myumbo wa uchumi
kimataifa. Wajumbe wamekazia kwamba, kazi ni nyenzo muhimu katika kulinda na kudumisha
utu na heshima ya binadamu.