2014-04-30 08:28:53

Kanisa linaomboleza kifo cha Askofu mkuu Damiào Franklin wa Jimbo kuu la Luanda, Angola


Askofu mkuu Damiào Antònio Franklin wa Jimbo kuu la Luanda, Angola, aliyekuwa na umri wa miaka 63 amefariki dunia, hapo tarehe 28 Aprili 2014, akiwa nchini Afrika ya Kusini, alikokuwa amelazwa kwa takribani mwezi mmoja hivi. Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Luanda inaomboleza kifo cha Askofu mkuu Franklin.

Itamkumbukwa kwamba, Marehemu Askofu mkuu Damiào Franklin alizaliwa kunako tarehe 6 Agosti 1950. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja takatifu la Upadre kunako mwaka 1978. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1992 akamteuwa kuwa ni Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Luanda, Angola na kunako mwaka 2001 akampandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Luanda, Angola.

Marehemu Askofu mkuu Franklin anakumbukwa na wengi kutokana na mchango wake wakati wa maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika, iliyofanyika mjini Vatican kunako mwaka 2009, kwani Marehemu Askofu mkuu Franklin alikuwa ni Katibu wa Kardinali Peter Turkson, ambaye kwa sasa ni Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani. Mipango ya mazishi inaendelea kufanyika Afrika ya Kuini na katika Jimbo kuu la Luanda, Angola.







All the contents on this site are copyrighted ©.