Haki, amani na upatanisho ni mchakato unaohitaji ushirikiano wa dhati!
Askofu Gervas Nyaisonga aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa
Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mpanda anasema kwamba, rushwa inabomoa msingi wa haki
na amani na kwamba, kuna haja kwa Kanisa kuendelea kushirikiana na wataalam, vyombo
vya habari na serikali ili kufichua vitendo vya rushwa, ili hatimaye, kujenga utawala
wa sheria, haki na amani.
Askofu Nyaisonga
katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, Kanisa linahitaji kushirikiana
na wadau mbali ili kujenga na kudumisha misingi ya ukwel, uwazi, uadilifu na uwajibikaji.
Wataalam wafanye tafiti za uhakika ili kubainisha mianya ya rushwa, ili kuweza kujenga
hoja ya nguvu katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, vinginevyo, mapambano haya
yanageukwa kuwa ni majungu.
Ili kuimarisha upatanisho na umoja wa kitaifa,
Jamii inapaswa kujielekeza katika kujitambua na kujikubali, tayari kuanza mchakato
wa pamoja katika kulinda na kudumisha mafao ya wengi badala ya kukumbatia misimamo
binafsi au ya vikundi ambayo wakati mwingine inaweza kuwa na madhara makubwa katika
Jamii.
Askofu Gervas Nyaisonga anasema, haki, amani na upatanisho ni mchakato
unaohitaji ushirikiano na mshikamano na wadau mbali mbali, ili kujenga msingi wa umoja
na mshikamano wa kitaifa, vinginevyo wananchi wanaweza kutawaliwa na hofu na wasi
wasi zisizo na msingi.