2014-04-29 09:51:30

Wabunge tekelezeni dhamana yenu kwa uadilifu mkubwa!


Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma wametakiwa kutekeleza dhamana hii nyeti na tete waliyokabidhiwa na watanzania wenzao kwa kuzingatia: umoja na mshikamano wa kitaifa; ustawi na maendeleo ya watanzania wengi; utu na heshima ya binadamu. Wabunge watekeleze kazi hii kwa kusukumwa na uzalendo na kamwe wasikumbatie misimamo na mawazo finyu ambayo hayana mashiko kwa ustawi na maendeleo ya Tanzania katika ujumla wake.

Kazi ya kutunga Katiba si nyepesi, inahitaji weledi, subira, ari na moyo wa kujadiliana kwa kuheshimiana na kuthaminiana, daima wakitarajia kuongozwa na neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili waweze kuchagua yaliyo mema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote. Ni ushauri uliotolewa hivi karibuni na Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mpanda, alipokuwa anazungumza na Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa, mjini Dodoma.

Askofu Gervas Nyaisonga ambaye kwa sasa anajiandaa kwenda Jimboni Mpanda kukabidhiwa Jimbo rasmi, anasema kuna haja kwa Wabunge kuheshimiana na kushirikishana mawazo katika mchakato wa kuandika Katiba bora zaidi, itakayokuwa na mafao na mashiko kwa watanzani kwa miaka mingi ijayo. Kamwe wasikate tamaa kwani inaonekana kuna baadhi ya Wabunge wamekwisha anza kukata tamaa kutokana na kile wanachokiona kikiendelea ndani ya Bunge mjini Dodoma.

Wabunge wasisite kutafuta ushauri makini kutoka kwa watanzania wenzao walioko nje ya Bunge, kwa ajili ya kupata Katiba bora itakayokuwa ni sheria mama, dira na mwongozo kwa watanzania wote. Kwa vile hili ni jambo nyeti na tete linalogusa maisha ya watanzania wote, halina budi kufanywa kwa kuomba maongozi ya Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala. Askofu Gervas Nyaisonga ametumia fursa hii kufungua Jumuiya ya Kikristo ya Watumishi wa Bunge na Wabunge inayojulikana kama Thomas Moore.







All the contents on this site are copyrighted ©.