2014-04-29 08:30:04

Papa Francisko anawaalika vijana kutoka kimasomaso kukutana na Yesu Mfufuka!


Vijana wanaalikwa kumwangalia kwa namna ya pekee kabisa yule kijana tajiri anayesimuliwa kwenye Maandiko Matakatifu aliyemwendea Yesu akiomba ushauri ili aweze kuurithi uzima wa milele. Mitume wengi walikuwa ni vijana na walifurahia sana walipokutana na kuzungumza na Yesu, kiasi hata cha kuwabadilishia mwelekeo wa maisha, kwani waliweza kusikiliza ufafanuzi wa Neno la Mungu kwa kina na mapana!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa video kwenye maadhimisho ya Siku ya Vijana Kikanda nchini Argentina, iliyoadhimishwa, Jumamosi tarehe 26 Aprili 2014 nchini Argentina, katika mkesha wa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu, anawauliza vijana, jinsi walivyojisikia kwa mara ya kwanza walipokutana na Yesu katika hija ya maisha yao ya kiroho, Anawaalika kuwaangalia Mitume waliokutana na Yesu kwa mara ya kwanza katika maisha yao.

Yesu alionesha upendo wa pekee kwa yule kijana tajiri aliyejitahidi katika maisha yake kushika Amri za Mungu, lakini akakosa ndani mwake ufukara wa maisha ya kiroho, ndiyo maana anapoambiwa kwenda kuuza vyote alivyonavyo na kuwapatia maskini, kisha amfuate Yesu, anashikwa na huzuni kubwa katika moyo wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maandiko Mataktifu yamesheheni mifano ya vijana wa kila aina. Anawakumbusha yule kijana aliyeomba urithi kutoka kwa Baba mwenye huruma, kisha akatokomea mjini kwenda kuponda mali na baadaye akakiona cha mtema kuni kwa kukumbana uso kwa uso na baa la njaa! Hapa akajifunza kutubu na kuongoka, ili kukimbilia tena huruma ya Mungu. Daima Baba yake alikuwa anamsubiri kwa hamu kubwa, kuona kijana wake akirudi tena nyumbani. Siku ile aliporejea nyumbani, akamkumbatia na kumwonjesha tena huruma na upendo usiokuwa na kifani.

Baba Mtakatifu amewakumbusha vijana wa Argentina kuhusu yule kijana wa Naini aliyekuwa amefariki dunia baadaye akafufuliwa na Yesu, kwa kumwonea yule mama mjane huruma? Baba Mtakatifu anawauliza vijana wao wanajisikia kuwa sehemu gani kati ya vijana wanaosimuliwa kwenye Injili? Je, wanaonesha ari na shauku ya kuwashirikisha wengine ushuhuda wa kukutana na Yesu? Au wamekata tamaa na kujikunyata? Au pengine tayari wamekwisha kupoteza maisha ya kiroho ndani mwao?

Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha vijana kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kutolea ushuhuda wa imani katika matendo, ili kujenga na kuimarisha amani na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake sanjari na kukumbatia Injili ya maisha pamoja na kuguswa na mahangaiko ya wengine kama alivyofanya Bikira Maria kwenye arusi ya Kana na mwishoni akasimama chini ya Msalaba wa Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wasichana kuiga mfano wa Bikira Maria na wanawake watakatifu wanaosimuliwa katika Injili kwa kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, wakimwachia Yesu nafasi ya kuwaongoza, ili waweze kukua na kukomaa, tayari kuwahudimia Watu wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu amewatakia kheri na baraka vijana hao katika maadhimisho ya Siku ya Vijana wa Argentina Kikanda, ili wapate nafasi ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao, bila kuwa na woga wala makunyanzi, bali wawangalie Yesu na Bikira Maria, ili waweze kusonga mbele, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.