Mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ghana
Askofu mkuu Jean Marie Speich, Balozi wa Vatican nchini Ghana, hivi karibuni aliwasili
nchini Ghana na kupokelewa na viongozi wa Kanisa na Serikali nchini humo baadaye kuhudhuria
hafla fupi ya “Akwaba” kadiri ya mapokeo ya wananchi wa Ghana.
Tarehe 27
Januari 2014 Askofu mkuu Speich aliwasilisha nakala za hati zake za utambulisho na
kupokelewa na Naibu Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ghana, Bwana Kwesi Quartey.
Viongozi hao wawili wamepongeza mchango wa Kanisa katika kuleta maendeleo kwa wananchi
wa Ghana katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Serikali ya Ghana imepongeza
ubora wa elimu na wainjilishaji wanaojitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi
wa Kanisa na maendeleo ya watu wa Ghana. Serikali inampongeza Baba Mtakatifu Francisko
kwa unyofu na jitihada zake za kuwa ni sauti ya wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii.
Tarehe 28 Januari 2014, Askofu mkuu Jean Marie Speich aliwasilisha
hati zake za utambulisho kwa Rais wa Ghana Bwana John Draman Mahama, baada ya kumkaribisha
kwenye Ikulu ya Ghana. Rais amewashukuru na kulipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki
Ghana kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, utu na heshima
ya binadamu bila kusahau ustawi na mafao ya wengi.
Askofu mkuu Jean Marie Speich
amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Rais na
wananchi wa Ghana katika ujumla wao. Baba Mtakatifu ameipongeza Ghana kwa kumteuwa
Balozi mkazi atakayeshughulikia masuala ya Ghana mjini Vatican.
Lengo ni kuendelea
kushirikiana na wadau mbali mbali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa
Ghana kwa sasa na kwa siku za usoni. Askofu mkuu Speich anasema, uwepo wake nchini
Ghana kama Balozi wa Vatican ni kuendeleza mchango wa Kanisa katika kulinda na kutetea
utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu pamoja na kujikita
katika mchakato wa maendeleo na ustawi wa wananchi wote wa Ghana.
Tarehe 6
Februari 2014, Askofu mkuu Speich alikutana na viongozi wakuu wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Ghana pamoja na kuwasilisha barua ya utambulisho kutoka kwa aliyekuwa Askofu
mkuu Pietro Parolin, katibu mkuu wa Vatican ambaye hivi karibuni alisimikwa rasmi
kuwa ni Kardinali. Baadaye Askofu mkuu Speich alitembelea Majimbo makuu yanayounda
Kanisa Katoliki Ghana kwa kukutana na kuzungumza na Maaskofu wakuu pamoja na waamini
wao.