2014-04-29 11:56:34

Kila mwananchi ana dhamana kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli!


Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mpanda, Tanzania katika mahojiano na Radio Vatican anakazia umuhimu wa Mama Kanisa, Serikali na Jamii kwa ujumla wake, kukazia umuhimu wa haki, amani na upatanisho wa kweli, kwani utapanisho na haki ni msingi ya amani ya kweli! RealAudioMP3

Amani ya kweli inajikita katika haki, upendo na mshikamano wa dhati na kwamba, upatanisho ni jambo linalotangulia masuala ya kisiasa, kwani hii ni nguvu inayopata chimbuko lake kutoka katika undani wa mtu. Ni jukumu la kila mwananchi kujikita katika kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho pamoja na kujenga mifumo itakayoimarisha misingi hii katika Jamii. Upendo wa kweli kati ya watu ni chemchemi ya amani.

Jamii haina budi kujikita katika ujenzi wa utawala bora unaozingatia sheria na kanuni za nchi. Ikiwa kama Serikali zinashindwa kudhibiti migogoro midogo midogo kuna hatari kwamba, haki na amani inaweza kutoweka na hivyo kusababisha majanga katika jamii ya watu. Kero na migongano kati ya wakulima na wafugaji ni mambo yanayopaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa!

Kashfa za kidini na ushabiki wa kisiasa anasema Askofu Nyaisonga ni mambo yanayoweza kusababisha kutoweka kwa misingi ya haki na amani. Kila mwananchi ana wajibu wa dhamana ya kukuza na kuendeleza misingi ya haki, amani na upatanisho.







All the contents on this site are copyrighted ©.