2014-04-29 09:33:52

Hospitali ya Mtakatifu Yohane Paulo II


Kanisa Barani Afrika limefuatilia kwa umakini mkubwa ushuhuda wa maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo wa pili aliyesimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, unaosimikwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Hizi ni juhudi ambazo hazina budi kulindwa na kuendelezwa kama njia ya kuenzi mchango wa Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili katika kudumisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Askofu Anthony Mukobo wa Jimbo Katoliki la Isiolo, Kenya amekubali kimsingi wazo la kuipatia Hospitali ya wanawake na watoto Jimboni humo, jina la Mtakatifu Yohane Paulo II. Hili ni wazo lililojitokeza kunako mwaka 2005 mara tu baada ya kifo cha Papa Yohane Paulo II, aliyependwa na wengi, kutokana na mchango wake katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, si tu kwa maneno matupu, bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake. Ni kiongozi aliyepokea mateso na kuyapatia maana mpya kwa kuimarisha imani na matumaini.

Hospitali ya Mtakatifu Yohane Paulo II, inatoa huduma kwa Mama na Mtoto katika Jimbo la Isiolo, Kenya. Huduma hii inapania pamoja na mambo mengine kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Kwa kuwa na usafiri wenye uhakika, wanawake wenye matatizo ya kijufungua wanaweza kukimbizwa mara moja kwenye Hospitali kubwa ili kuokoa maisha ya Mama na mtoto. Juhudi hizi hazina budi kwenda sambamba na maboresho ya miundo mbinu, kwa kuwa na usafiri wenye uhakika na salama kwa wanawake wajawazito.

Hospitali ya Mtakatifu Yohane Paulo II imeanza kuwa mstari wa mbele kwa kutoa huduma makini kwa Mama na Mtoto vijijini sanjari na kuwaandaa wakunga wa jadi wanaosimamiwa na kupewa mafunzo na wauguzi waliobobea, ili kuendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wanawake wajawazito vijijini. Inasikitisha kuona kwamba, wanawake wengi wanapoteza maisha wakati wa kujifungua, hali ambayo inachangia ongezeko la vifo vya wanawake wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Takwimu zinaonesha kwamba, wanawake wanaoishi katika Nchi zinazoendelea duniani wanapata mimba kwa wingi ikilinganishwa na wanawake wanaoishi katika Nchi tajiri zaidi duniani, ambao wengi wao kwa sasa mambo ya uzazi hayana tena msukumo wa pekee, bali wanataka kuponda mali na kuvinjari maisha. Kuna haja ya kufanya maboresho ya huduma ya Mama na mwana kwenye kambi za wakimbizi, kwa kutambua umuhimu wa wanawake katika kuchangia ustawi na maendeleo ya nchi zao.

Watetezi wa haki msingi za wanawake wanasema, kuna haja kwa jamii kudhibiti vitendo vya unyanyasaji na dhuluma dhidi ya wanawake kwa kuwapatia haki zao msingi pamoja na kuthamini utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanawake wasaidiwe kiroho na kimwili, ili waweze kutekeleza dhamana na utume wao ndani ya Jamii na Kanisa katika ujumla wake. Wanawake wakiwezeshwa kwa njia ya elimu makini na uchhumi endelevu, wanaweza kusaidia katika mchakato wa maboresho ya familia na jamii inayowazunguka.







All the contents on this site are copyrighted ©.