2014-04-29 07:49:41

Endelezeni urithi wa Mtakatifu Yohane XXIII katika uhalisia wa maisha yenu!


Mtakatifu Yohane XXIII alipadrishwa kunako tarahe 19 Machi 1925 kwenye Kanisa la Watakatifu Ambrose na Carlo mjini Roma. Jumatatu tarehe 28 Aprili 2014, waamini kutoka Jimbo Katoliki la Bergamo, Kaskazini mwa Italia, waliokuwa wamemiminika kwa wingi kushuhudia Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II wakitangazwa kuwa Watakatifu, jumapili iliyopita, wamehudhuria Ibada ya Misa ya shukrani kwa zawadi kubwa ya watakatifu jasiri waliowaonjesha watu huruma ya Mungu.

Ibada hii imeongozwa na Kardinali Gionigi Tettamanzi, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Milano na mahubiri kutolewa na Askofu Francesco Beschi wa Jimbo Katoliki la Bergamo, ambaye amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu, matendo makuu ya Mungu kati ya watu wake.

Tukio hili la imani linaongeza matumaini yanayobubujika kutoka katika Injili ya Kristo na mwanga angavu wa ushuhuda uliotolewa na Mashahidi wa Kristo, changamoto na mwaliko kwa waamini kupokea matunda yanayochipuka kutoka kwa utakatifu wa maisha, ili kila mtu na kila jumuiya iweze kuyafanyia kazi.

Askofu Beschi anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe alioiandikia Familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Bergamo kupitia gazeti lake la Eco, kwa kusema kwamba, yamewatia ari na moyo mkuu, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini kwa kuendeleza urithi wa maisha ya kiroho ulioachwa na Mtakatifu Yohane XXIII, ambaye alizaliwa, akakulia na kuishi Jimboni humo. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake huo, alikuwa amekazia mambo makuu matatu.

Mosi, kuendeleza urithi na kumbu kumbu ya utakatifu wa Yohane XXIII na kuumwilisha katika uhalisia wa maisha ya mtu binafsi, familia na jumuiya ya waamini, kwa kuonesha upendo kwa Yesu na Kanisa lake, katika moyo wa udugu na mshikamano wa dhati. Askofu Beschi anasema, tukio la kuwatangaza Watakatifu hawa wapya ni changamoto ya kuendelea kukuza na kuimarisha imani na kwamba, huu ni utajiri mkubwa katika maisha yao ya kiroho.

Pili ni kupokea mabadiliko yaliyoletwa na Mtakatifu Yohane XXIII kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kutolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Injili ya Kristo pamoja na kuendelea kuwa wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, kama alivyojitahidi kufanya Mtakatifu Yohane XXIII.

Tatu, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kuendeleza hija ya mageuzi yaliyoletwa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kuwajibika na kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya waamini katika ulimwengu mamboleo. Huu ni mwaliko pia wa kuendeleza mshikamano wa upendo na udugu kati ya watu.

Hivi ndivyo waamini kutoka sehemu mbali mbali wanavyoendelea kumshukuru Mungu kwa zawadi ya miamba wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo!







All the contents on this site are copyrighted ©.