Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini katika maadhimisho ya Siku kuu ya Vasakh
inayoadhimishwa na waamini wa dini ya Kibudha, kila mwaka ifikapo tarehe 6 Mei huko
Asia Mashariki ambayo pia husherehekewa sehemu mbali mbali za dunia kati ya tarehe
13 na tarehe 14 Mei ya kila Mwaka. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya ni: “Wabudha
na Wakristo kwa pamoja wajitahidi kujenga udugu”.
Ni kauli
mbiu inayopata chimbuko lake kutoka kwenye ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa
ajili ya kuombea amani duniani kwa Mwaka 2014, aliyekazia kwamba, udugu ni msingi
na njia ya amani. Udugu ni kigezo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu kinachomwezesha
mtu kumthamini na kumhudumia jirani yake kama binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano
wa Mungu. Huu ni msingi wa ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika msingi wa haki na amani
ya kudumu.
Uhusiano wa kidini unaojengeka katika misingi ya urafiki, majadiliano,
ukarimu na mapendo ya dhati ni mambo ambayo yanajenga na kuimarisha mahusiano ya kidugu.
Mzizi mkuuwa fitina na chuki ni ujinga unaosababishwa na waamini kutofahamiana kwa
dhati na kwamba ubinafsi umekuwa ni chanzo cha vita na uvunjifu mkubwa wa haki msingi
za binadamu. Mambo haya yanasababisha watu kutoonana na kupendana, ili kujenga na
kuimarisha umoja.
Wabudha na Wakristo wanaishi katika ulimwengu ambamo bado
kuna dhuluma, ubinafsi, ukabila, kinzani za kikabila, vita, misimamo mikali ya kiimani,
hali ya baadhi ya watu ndani ya Jamii kujisikia wanyonge au kuonekana kuwa ni tisihio
na hivyo kuwa ni sababu ya kuondolewa kwao kutoka katika uso wa dunia. Waamini wanahamasishwa
kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, ili kuheshimu na kuendeleza msingi wa
maisha ya binadamu katika medani mbali mbali za maisha.
Waamini kwa pamoja
wanapaswa kusimama kidete kukemea dhambi za kijamii zinazoathiri udugu; kujitahidi
kuwa ni wajenzi wa ukarimu na wadau wa upatanisho, wanaojitahidi kuvunja kuta za utengano
ndani ya Jamii ili kujenga na kuimarisha Jamii inayosimikwa katika udugu kati ya mtu
mmoja mmoja na makundi ya watu.
Duniani kuna mambo yanayowaunganisha watu katika
utu na heshima yao kama binadamu na hivyo wanashiriki katika mchakato wa ujenzi wa
dunia inayosimikwa katika haki, amani na udugu, jambo linalohitaji utambuzi wa pamoja
wa tunu hizi msingi. Majadiliano ya kidini ni njia muafaka ya kutambua na kuenzi tunu
hizi zinazojikita katika maadili, ili kujenga umoja na udugu kama sehemu ya Familia
ya binadamu.
Kila mwamini anachangamotishwa kuwa ni mjenzi wa amani kwa kukataa
katu katu sera za chuki, ili kujenga ulimwengu unaojikita katika utamaduni wa majadiliano
na kukutana na watu. Juhudi hizi hazina budi kujikita katika malezi, hasa miongoni
mwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kuwa na ujasiri wa kujenga udugu. Baraza la
Kipapa linahitimisha ujumbe wake kwa waamini wa dini ya Budha kwa kuwatakia Siku kuu
njema ya Vasakh, ili kweli iwe ni fursa ya kuendeleza udugu katika Jamii ambazo bado
zimegawanyika. Ujumbe huu umetiwa sahihi na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza
la Kipapa la Majadiliano ya kidini.