2014-04-28 08:51:34

Padre Giuseppe Girotti atangazwa kuwa Mwenyeheri!


Kardinali Severino Poletto kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe 26 Aprili 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Giuseppe Girotti kuwa ni Mwenyeheri. Huyu ni Padre Mdonikani aliyeishi kati ya Mwaka 1905 hadi mwaka 1945. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Alba, Kaskazini mwa Italia. RealAudioMP3

Mwenyeheri Girotti aliuwawa kikatili kwa kudungwa sindano yenye sumu, wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kunako Mwaka 1945. Hata alipokuwa gerezani wafungwa wenzake walitambua utakatifu wa maisha yake, kiasi cha kuandika kwenye kuta za gereza "Mtakatifu Giuseppe Girotti".

Alikamatwa na utawala wa kinazi tarehe 29 Agosti 1944 huko Torino, Kaskazini mwa Italia, akafungwa kwenye kambi ya mateso ya Dachau. Hiki kilikuwa ni kipindi cha mateso na mahangaiko ya watu; dhuluma na nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Katika kipindi hiki, hata Mapadre nao walikiona cha mtema kuni!

Padre Giuseppe Girotti alihukumiwa kifo kutokana na chuki za kidini, kwani alituhumiwa kwamba, alikuwa anawahudumia watu wote, wakiwamo Wayahudi bila ya ubaguzi, jambo ambalo lilimpelekea kuhukumiwa kifo chenye maumivu makali na cha pole pole kama vile mshumaa unavyowaka na kuteketea. Hii ilikuwa ni Njia ya Msalaba na mateso makali kwa Mwenyeheri Giuseppe Girotti. Akavumilia mateso yote haya kwa imani thabiti bila hata ya kuteteleka, akajitahidi kumwiga Yesu Kristo katika Njia yake ya Msalaba, hadi pale nguvu zilipomwishia na kukata roho!

Alipokuwa gerezani, kila siku asubuhi alijitahidi kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Mapadre wenzake waliokuwa wamefungwa pamoja naye. Alipopata fursa kidogo ya mapumziko, alisoma na kutafakari Maandiko Matakatifu. Mwenyeheri Girotti alikuwa ni mtaalam na bingwa wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu, aliyependa kurutubisha umoja miongoni mwa Wakristo na kulaani vita iliyokuwa inasababisha maafa makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia!

Mwenyeheri Giuseppe Girotti alilipenda Kanisa na akaona mchango wake katika medani mbali mbali za maisha ya watu, kwa kukazia na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu. Aliona kwamba, Kanisa lilikuwa ni kimbilio la wengi katika shida na mahangaiko yao ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Utume huu unaweza kutekelezwa zaidi, ikiwa kama Wakristo wote watakuwa wameungana pamoja katika umoja na mshikamano wa dhati. Lakini, alisikitika kuona kwamba, bado Wakristo walikuwa wamegawanyika, kinyume kabisa cha utashi na sala ya Kristo, ili wote wawe wamoja!

Mwenyeheri Giuseppe Girotti alizaliwa mjini Alba kunako mwaka 1905. Akajiunga na Shirika la Wadominikani kunako mwaka 1919 na kuweka nadhiri za kwanza mwaka 1923. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kikasisi, akapadrishwa kunako tarehe 3 Agosti 1930. Kati ya mwaka 1931 hadi mwaka 1934 alirudi shuleni kujinoa katika masomo kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, Roma na baadaye mjini Yerusalemu. Kati ya mwaka 1935 hadi mwaka 1938 alifundisha mjini Torino.

Katika Maandiko Matakatifu alijitahidi kumtafuta Mungu na akabahatika kukutana naye. Alikuwa na utaalam wa kufundisha Maandiko Matakatifu, kiasi cha kugusa undani wa maisha ya watu, kwa njia ya mifano ya maisha yake!







All the contents on this site are copyrighted ©.