2014-04-28 14:08:49

Mtakatifu Yohane Paulo II alitetea Injili ya Familia, Uhai na akaonesha Ibada kwa Bikira Maria


Miaka tisa imekwisha yoyoma tangu Yohane Paulo II alipofariki dunia, umati mkubwa wa Familia ya Mungu, ukashuhudia jinsi ambavyo, Yohane Paulo II alivyokuwa mtii katika Injili ya Kristo, kiasi kwamba, alijitosa bila ya kujibakiza ili kuitolea ushuhuda Injili ambayo ni mwanga na matumaini kwa Wakristo wa vizazi vyote.

Mama Kanisa ametambua utakatifu wa Yohane Paulo II, changamoto na mwaliko wa kujitahidi kutoa mfano wa maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Ni kiongozi aliyethubutu kuwatangazia walimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake uwepo wa Kristo kati ya watu wake. Aliwainjilisha watu kwa njia ya mateso na mahangaiko yake, akawaonjesha imani thabiti inayojikita katika Fumbo la Msalaba, kiasi kwamba, imani yake ikang'aa katika giza na wasi wasi wa maisha ya watu!

Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Angelo Comastri katika Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa Mama Kanisa kuwatangaza watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa Watakatifu. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 28 Aprili 2014.

Mtakatifu Yohane Paulo II alisimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya kifamilia dhidi ya sera na mikakati iliyokuwa inalenga kubomoa taasisi ya familia. Mama Kanisa anatambua umuhimu wa familia katika Jamii, ndiyo maana anaendelea kutangaza ukuu wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema kwamba, Familia ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inapaswa kulindwa na kudumishwa hata kama ni kwa kujisadaka kwa njia ya maisha, kama ilivyotokea kwake, ili walimwengu waweze kusoma na kuitafakari Injili ya mateso ya familia, kama maandalizi makini ya kulinda na kuitetea familia katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Mtakatifu Yohane Paulo II alisimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatia sera za utoaji mimba, ubinafsi na hali ya kutojali wala kuguswa na utakatifu wa maisha. Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na Ibada kubwa kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, ndiyo maana alipenda kumkabidhi Injili ya Uhai, ili aweze kusaidia kulinda na kuwaombea watu waliokuwa wanateseka kwa kutolewa mimba, vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya wasichana na wanawake pamoja na kifo laini.

Mtakatifu Yohane Paulo II alikemea vita kwa nguvu zote kwa kuwakumbusha wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kwamba, vita inasababisha mateso na majanga katika maisha ya watu wengi na kamwe haiwezi kuleta suluhu ya matatizo yanayojitokeza katika uso wa dunia. Hizi ni dalili za binadamu kutembea katika utupu, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumkimbilia Yesu Kristo ili aweze kuwapatia utimilifu wa maisha.

Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, walimtambua Mtakatifu Yohane Paulo II kama Baba, rafiki na mlezi. Alionesha, uaminifu, furaha na ukamilifu wa maisha na utume wa Kipadre wakati wa kinzani na utepetevu wa maisha na maadili ya Kipadre kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kwa hakika aliwasaidia waamini wengi kujenga na kukuza Ibada kwa Bikira Maria baada ya mtikisiko uliosababishwa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II anatambua kwamba, ni kwa msaada na ulinzi wa Bikira Maria aliweza kunusurika na kifo siku ile ya tarehe 13 Mei 1981, akajiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria kwa maneno haya "Totus tuus". Kwa ufupi anasema Kardinali Angelo Comastri, huyu ndiye Mtakatifu Yohane Paulo II







All the contents on this site are copyrighted ©.