Mpendwa Msikikizaji wa Radio Vatikani, karibu kwa mara nyingine tena katika kipindi
chetu cha Kanisa la Nyumbani. Tunaendelea kuungana na Mama Kanisa kumshukuru Mungu
kwa zawadi ya Watakatifu Yohane Paulo II na Yohane wa XXIII, walioandikwa karika Orodha
ya Watakatifu na kutangazwa rasmi katika Dominika ya Huruma ya Mungu.
Ni neema
ya pekee mpendwa msikilizaji, kushuhudia watu hawa walioishi nyakati zetu, waliotugusa
kwa maadhimisho ya neno na Sakramenti kama makuhani wa Bwana, na zaidi walioliongoza
Kanisa la Mungu katika hija yake hapa duniani. Hivyo tumeshuhudia maisha yao, wito
wao, kazi na jasho lao, na tulishuhudia jinsi walivyompendeza Mungu na zaidi sana
tunashuhudia jinsi wanavyoandikwa katika orodha ya watakatifu.
Ni heri kubwa
kwetu kushuhudia mambo haya. Basi nasi tukijawa hamu ya kushiriki karamu ya wateule
mwisho wa uzima huu, tunahimizwa, tunatiwa moyo kwa mfano wa maisha yao. Na katika
hili tunazidi kuaminishwa ya kwamba, utakatifu inawezekana. Neno la Mungu linatualika
sote, likisema “Wakumbukeni viongozi wenu waliowahubirieni Neno la Mungu. Fikirini
juu ya mwenendo wao, mkaiige imani yao”. Hebr. 13:7
Katika kipindi hiki tutafakari
kwa uchache juu ya wito wa kuwa mtakatifu. Kwa mwangwi wa mafundisho ya Kanisa, sisi
sote tumeitwa kuwa watakatifu (Rejea Sheria ya Kanisa, na 210, Hati ya Mtaguso – Mwanga
wa Mataifa nn 39-40). Utakatifu sio kitu ambacho mtu hupewa baada ya kufa, hapana.
Utakatifu ni hali nzima ya maisha ambayo mtu hujibidisha kuitafuta na kuiishi duniani
hapa na mwisho kushirikishwa uzima ule wa milele mbinguni.
Sisi tulio hai,
tumeitwa kuwa watakatifu na pia tunatamani, mwisho wa maisha yetu haya, tukaunganika
na Kanisa la Watakatifu huko mbinguni. Tuwapo hapa duniani, tunasafiri (ndiyo maana
tunaitwa Kanisa linalohiji), tunapigana vita vya kiroho na kimwili. Na kwa msaada
wa Neno la Mungu, Sakramenti, sala, Ibada, Liturujia, matendo ya upendo kwa Mungu
na jirani, tunatazamia mwisho ule mwema, yaani muungano kamili na Mungu aliye lengo-kikomo
letu. Mwisho wa jitihada zote tunatamani tukamwone Mungu, tukaishi naye milele.
Watakatifu
ni nani? Ni watu ambao, walipokuwa hapa duniani walimpendeza Mungu kwa maisha yao.
Walijibidisha kumjua Mungu wa kweli, kumpenda na kumtumikia. Na baada ya kuondoka
kwao katika uzima huu, Mungu ameendelea kutenda kazi ndani mwao na kwa njia yao, kwa
ishara na miujiza mbalimbali, inayodhihirisha nguvu hiyo ya Mungu. Kwa sababu ya maisha
yao na ishara hizo, Mama Kanisa Mtakatifu, kwa uongozi wa Mungu mwenyewe, anawaandika
rasmi katika orodha ya Watakatifu.
Kumtangaza mtu kuwa mtakatifu ni MCHAKATO.
Mchakato huu unaongozwa na Imani Takatifu, taratibu-kanuni za jumla na za kipekee.
Mama Kanisa anazo taratibu maalumu za kufuata hata mtu aliyeitwa kutoka dunia hii,
aweze kutangazwa kuwa mtakatifu. Tunapotafakari juu ya zawadi ya watakatifu wetu
wapya, tujulishane kwa ufupi hatua zinazofuatwa hadi mtu aweze kutangazwa kuwa mtakatifu.
Baada
ya kufariki mtu, na kisha kuona baadhi ya ishara na miujiza, inayosindikizwa na aina
ya maisha ambayo huyo mtu aliishi na aina ya kifo alichokufa, kisha kupita miaka mitano
baada ya kufariki, ndipo wahusika huweza kuanza kuomba ruhusa kutoka kiti kitakatifu
ya kuanza mchakato wa kumtangaza mtu kuwa ni mtakatifu. Ruhusa hiyo huweza kuombwa
na wanandugu au kundi la waamini, au shirika la kitawa kama alikuwa mtawa. Ruhusa
hiyo inaombwa kupitia kwa askofu Jimbo, kule alikoishi au kufia mtu huyo. Kiti kitakatifu
kikishakutoa ruhusa kwamba mchakato uendelee, basi kwa uruhusisho huo huyo aliyefariki
haitwi tena marehemu, bali ni MTUMISHI WA MUNGU.
Baada ya uruhusisho huo,
kamati maalumu ya watu wenye imani thabiti na wenye kujua thamani ya ukweli mbele
ya Mungu, huanza kukusanya ushahidi juu ya maisha ya MTUMISHI WA MUNGU. Hapa kuna
ushahidi wa maandishi kama aliyaacha, maneno aliyokuwa anatamka (masimulizi kutoka
kwa watu), matendo yake ya kiimani kama vile maisha ya sala, sadaka na majitoleo;
matendo yake ya upendo kwa jirani. Hayo yote hukusanywa na kuhakikiwa na ile kamati
maalumu ngazi ya jimbo. Nayo huwakilisha uhakiki wao tena kwa Askofu Jimbo. Askofu
jimbo ndiye mwenye wajibu msingi wa kuwaongoza waamini wake kwa Mungu.
Kisha
hakikiwa na Askofu Jimbo, taarifa zote za MTUMISHI WA MUNGU hupelekwa tena katika
Kiti Kitakatifu (katika ofisi maalumu inayohusika na kuwatangaza Watakatifu). Nako
huko taarifa hizo huhakikiwa kwa Kanuni maalumu zinazoongozwa na Imani kwa Mungu na
Kanisa lake katika Kristo Yesu. Taarifa hiyo ikiwa haina mawaa, hupelekwa kwa Baba
Mtakatifu, naye kwa uwezo wa kimungu kama Wakili wa Kristo na kwa mamlaka aliyo nayo,
huhukumu uhalali wa taarifa ya mtumishi wa mungu. Endapo taarifa hiyo itakuwa ni
matendo mema ya ushuhuda na ushujaa wa imani, basi Baba Mtakatifu ataidhinisha huyo
MTUMISHI WA MUNGU awe MHESHIMIKA. Na hivyo kanisa mahalia huweza kuanza tu kumheshimu.
Huyo
MTUMISHI MHESHIMIKA WA MUNGU, akitenda walao muujiza mmoja, muujiza huo huhakikiwa
na kamati ya Imani na WANASAYANSI, ili kuhukumu kuwa kweli ni muujiza, ni nguvu ya
mungu imetendeka, iwe katika uponyaji au jambo lolote. Muujiza huo hudhihiridha nguvu
ya Mungu inayotenda kazi kwa njia ya MTUMISHI MHESHIMIKA WA MUNGU. Taarifa hiyo ya
Muujiza, hupelekwa tena katika kiti kitakatifu. Kiti kitakatifu kikiridhia uhalali
wa muujiza au miujiza hiyo, hupeleka taarifa yote kwa Baba Mtakatifu. Na Baba Mtakatifu
naye kwa nguvu ya kimungu na uwezo aliopewa, huhukumu na kumtangaza mtumishi wa mungu
kuwa mwenyeheri.
Baada ya hapo, mchakato unaendelea wa kumtangaza MWENYEHERI
kuwa Mtakatifu. Hapo ndipo huhitajika muujiza mwingine tena. Hadi hapo Kiti kitakatifu
huweza kuruhusu Makanisa, Mashule na majengo mbalimbali kujengwa kwa heshima ya mwenye
heri huyo, na huku watu wakiendelea kuomba msaada wa sala na maombezi yake. Ukiongezeka
muujiza mwingine tena, na ukahakikiwa kwa mtindo uleule, hapo sasa mwenyeheri hutangazwa
kuwa ni mtakatifu. Hivyo baada ya kufa tuna hatua hizi: MTUMISHI WA MUNGU, MHESHIMIKA,
MWENYE HERI na mwisho MTAKATIFU. Hawa waliotangazwa Jumapili ya huruma ya Mungu, tarehe
27 Aprili 2014 WAMEPITIA HATUA HIZO ZOTE.
Kutangazwa kuwa mtakatifu ni tendo
la kiimani na kiibada, linalofanywa na BABA MTAKATIFU, tendo ambalo kwa asili na kwa
uvuvio wa Roho Mtakatifu, LIMEKINGWA NA KILA DOSARI, yaani KANISA KWA NJIA YA WATUMISHI
WAKE, haliwezi kumtangaza Mtakatifu mtu asiyestahili. Na kisha kutangazwa Mtakatifu
sasa, huyo hupewa tarehe maalumu ya kukumbukwa na Kanisa la Jumla, jina lake huandikwa
katika orodho ya watakatifu na waamini huwalikwa kumfanya awe mwombezi na mfano wa
maisha yake kuwa kielelezo cha maisha yetu ya kumtafuta Mungu.
Tunamwomba
Mungu, kwa Maombezi ya Watakatifu Yohane wa XXIII na Yohane Paulo wa Pili, tujaliwe
hali njema, tusafiri salama ili mwisho wa uzima huu, nasi tukamwone Mungu wetu. Kutoka
Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.