Waamini waliokuwa wamefurika mjini Vatican kwa ajili ya kushiriki Ibada ya Misa Takatifu
ya kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu, walifanya
kesha la sala na tafakari ya Neno la Mungu pamoja na mafundisho ya Wenyeheri Yohane
XXIII na Yohane Paulo II kwatika Makanisa mbali mbali Jimbo kuu la Roma. Ulikuwa ni
usiku wa mshikamano katika maisha ya kiroho, kwa kufanya toba na maungano ya dhambi,
tayari kushiriki katika Ibada ya Misa takatifu, Jumapili tarehe 27 Aprili 2014.
Pamoja
na hali mbaya ya hewa iliyojitokeza Jumamosi, Jioni, lakini bado makundi makubwa ya
waamini waliokuwa wakipeperusha bendera na kuimba nyimbo, yalionekana yakitembea kwenye
mitaa na viunga vya mji wa Roma bila wasi wasi, ili kushiriki: Ibada na Katekesi mbali
mbali zilizokuwa zinatolewa kwenye Makanisa. Baadhi ya waamini walilala karibu na
viunga vya Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ili kuhakikisha kwamba, wanashiriki
kwa ukaribu zaidi katika tukio hili la kihistoria, ambalo Mwenyezi Mungu ameliwezesha
Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.