2014-04-27 10:43:00

Mtakatifu Yohane XXIII: Uinjilishaji, Majadiliano na Amani!


Mtakatifu Angelo Giuseppe Roncali alizaliwa Bergamo, Kaskazini mwa Italia, tarehe 25 Novemba 1881 na kubatizwa siku hiyo hiyo. Alipata Kipaimara na Komunio ya kwanza kunako mwaka 1889 na mwaka 1892 akaingia Seminarini. Alikuwa na kipaji cha uandishi wa habari na makala zake zimekusanywa katika kitabu kinachojulikana kama "Giornale dell'anima". RealAudioMP3

Kati ya mwaka 1901 hadi mwaka 1905 alipelekwa kusoma kwenye Seminari kuu ya Kipapa, Jimbo kuu la Roma na baadaye, akaenda Jeshini kwa mujibu wa sheria. Tarehe 10 Agosti 1904 akapewa daraja takatifu la Upadre.. Mwaka 1905 akachaguliwa kuwa Katibu wa Askofu Giacomo Maria Radini Tedeschi hadi mwaka 1914. Akamsaidia Askofu wake katika kutekeleza utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Bergamo. Aliwahi pia kufundisha pamoja na kufanya marekebisho katika Katiba ya Vijana Wakatoliki Italia. Alikuwa anashiriki kuandika makala kwenye Gazeti la Jimbo Katoliki Bergamo na kwamba, alikuwa ni mhubiri mahiri na makini.

Katika tafiti zake alibahatika kukutana na watakatifu Charles Borromeo na Mtakatifu Francisko wa sale na kwamba, hiki kilikuwa ni kipindi cha mwamko na mikakati ya shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa. Askofu Radini Tedeschi akafariki dunia kunako mwaka 1914 na Padre Angelo Roncali akaendelea na utumishi wake wa Kipadre na mwalimu Seminarini.

Wakati Italia ilipotumbukia katika vita kunako mwaka 1914, aliitwa kuwa ni Padre wa maisha ya kiroho kwa Askari waliokuwa mstari wa mbele. Baada ya vita alifungua nyumba kwa ajili ya wanafunzi, ili kusaidia wanafunzi katika maisha yao ya kiroho. Kunako mwaka 1919 akateuliwa kuwani Padre wa maisha ya kiroho. hapa akafunga ukurasa wa maisha yake, sehemu ya kwanza.

Kunako Mwaka 1921 aliitwa mjini Vatican na Papa Benedikto wa kumi na tano, kama Rais wa Italia katika Baraza kuu la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Kunako mwaka 1925 Papa Pio XI akamteua kuwa Balozi wa Vatican nchini Bulgaria na hivyo kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu na kauli mbiu yake ilikuwa ni "Oboedientia et pax" "Utii na Amani", mambo aliyoyapatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake kama Askofu na baadaye kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Akawekwa wakfu kama Askofu hapo tarehe 19 Machi 1925. Akatembelea na kuimarisha Jumuiya za Kikristo nchini Bulgaria,

Tarehe 27 Novemba 1935 aliteuliwa kuwa ni Mwakilishi wa Vatican nchini Uturuki, akajitosa kimasomaso kwa ajili ya huduma ya Kanisa miongoni mwa vijana; akajenga na kuimarisha majadiliano ya kidini. Wakati wa Vita kuu ya Pili ya Dunia alijitahidi kuwasaidia watu wengi waliokuwa wanateseka. Tarehe 20 Desemba 1944 Papa Pio XII akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Ufaransa. Wakati wa vita aliwasaidia sana wafungwa wa kisiasa, akatekeleza utume wake katika hali ya unyenyekevu na akaendelea kuonesha utume wake kama Padre. Alikuwa kweli ni mtu wa sala na tafakari ya kina.

Tarehe 12 Januari 1953 akateuliwa kuwa Kardinali na tarehe 25 Januari akateuliwa kuwa Patriaki wa Venezia, akajitosa tena katika maisha ya kitume na shughuli za kichungaji, akaonesha ushupavu na utakatifu wa maisha katika kazi za kichungaji, huku akijitahidi kufuata mifano ya watangulizi wake hapo Venezia.

Baada ya kufariki dunia kwa Papa Pio XII akachaguliwa tarehe 28 Oktoba 1958 kuwa Papa na akaamua kutumia jina la Yohane XXIII, akajionesha ulimwenguni kama Mchungaji mwema; mnyenyekevu na mpole wa moyo, jasiri na mwenye huruma, aliyemwilisha matendo ya huruma katika utume wake, kwa kuwatembelea wagonjwa na wafungwa. Akakazia umuhimu wa Kanisa kuwa kweli ni Mwalimu na Mama kwa kuandika Waraka wa kichungaji, "Mater et Magistra" wa Mwaka 1961 na "Pacem in Terris" Amani Duniani mwa Mwaka 1963.

Aliitisha Sinodi ya Jimbo kuu la Roma, akaunda Tume ya kurekebisha Sheria za Kanisa na hatimaye, akaitisha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Akatembelea Parokia mbali mbali za Jimbo kuu la Roma, ili kuwaimarisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Ni kiongozi aliyejikita katika mchakato wa Uinjilishaji, majadiliano ya kiekumene pamoja na majadiliano na watu wote. Tarehe 3 Juni 1963 akafariki dunia kwa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, akasindikizwa na litania ya sala kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 3 Septemba 2000 wakati wa Maadhimisho ya Jubilee kuu ya Miaka Elfu mbili ya Ukristo akamtangaza kuwa Mwenyeheri. Jumapili tarehe 27 Aprili 2014 ametangazwa kuwa Mtakatifu, matendo makuu ya Mungu.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.