Jibidisheni zaidi kugundua utajiri unaofumbatwa katika Nyaraka za Mtaguso mkuu wa
Pili wa Vatican
Padre Raymond Saba, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano
maalum na Radio Vatican wakati huu Mama Kanisa anapomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi
wa sifa na shukrani kwa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa
watakatifu anasema, Yohane wa XXIII atakumbukwa sana na Kanisa Barani Afrika, lakini
na Tanzania kwa namna ya pekee. Ni Papa aliyemteua Askofu Laurian Rugambwa kuwa Kardinali
wa kwanza mwafrika, matendo makuu ya Mungu!
Wakati Tanganyika
inajiandaa kupata uhuru wake, Papa Yohane XXIII alimzawadia Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere Biblia ambayo hadi sasa inatunzwa Seminari kuu ya Kipalapala, Jimbo kuu la
Tabora, ili iweze kusaidia katika kuaongoza watanganyika kwa wakati huo, kwa hekima,
busara na kweli za Kiinjili. Leo hii, Jimbo Katoliki la Musoma, liko katika mchakato
wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Mwalimu Nyerere kuwa ni Mwenyeheri, kutokana na mfano
bora wa maisha kama mwamini mlei na mwanasiasa mahiri duniani.
Papa Yohane
XXIII ndiye aliyetunga Sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanzania na watu wake, ili
iweze kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati.
Tanzania anasema Padre Saba imezaliwa na kulelewa katika fukuto la maadhimisho ya
Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Maaskofu wazalendo saba kutoka Tanzania walihudhuria
maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yaliyokuwa yameitishwa na Papa Yohane
XXIII.
Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni chombo makini na dira rejea katika
maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Changamoto
ambayo bado iko mbele ya Familia ya Mungu ni kuendelea kujifunza kwa bidii zaidi Mafundisho
ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ili kugundua tena na tena utajiri unaofumbatwa
katika Nyaraka hizi.