Katika dominika hii ya pili ya Pasaka, Injili inatuletea aina mbili za mazingira yaliyo
tofauti:Mazingira ya kwanza, Yesu anawatokea wafuasi jioni ya siku ileile ya Pasaka,
wakiwa chumbani pindi mtume mmoja aitwaye Thomas hakuwepo. Mazingira ya pili, ni siku
nane baadaye Yesu anawatokea tena wafuasi chumbani sasa akiwepo hata Thomas. Mazingira
ya kutokea-tokea kwa Yesu baada ya ufufuko wake ni tofauti hasa ukikumbuka alivyomtokea
mara ya kwanza Maria Magdalena asubuhi ileile ya Pasaka.
Mazingira aliyomtokea
nayo yalikuwa ni ya nje kwenye bustani karibu na kaburi. Lakini kwa mitume ilikuwa
ni jioni tena chumbani milango ikiwa imefungwa kutokana na woga wa wanafunzi. Mwinjili
anataka kutuonesha kwamba Yesu anafika katika ulimwengu kwa namna ambayo si ya kiyakinifu,
ni yeye lakini siyo yuleyule. Kitu cha muhimu zaidi kukiepa hapa ni matumizi ya neno
hili “kutokea”, kwa sababu neno hili halijatumika kabisa na mwinjili. Fasuli inasema,
Yesu alikuja na kusimama katikati. “Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale
walipokuwa wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi: akaja Yesu akasimama
katikati, akawaambia, “Amani iwe kwenu.” (Yoh. 20:19).
Siku ya Pasaka na siku
nane baadaye Bwana anakuja na kukaa katika jumuia yake iliyokusanyika pamoja, na kama
ilivyokuwa kwa wafuasi wale wa mwanzo siku ya Pasaka kadhalika waumini siku ya Pasaka.
Waumini hao hawana budi kufungua sana macho yao, lakini siyo macho ya kiyakinifu,
yanayoangalia kwa udadisi na kuanisha mambo, bali kwa macho safi, macho ya imani yanayoweza
kuona mambo yasiyoweza kuonekana kwa macho ya kawaida.
Ndivyo inavyotufundisha
Injili ya leo jinsi ya kufungua macho ya imani na kuangalia Yesu mfufuka anayefika
na kukaa kati ya jumuia iliyokusanyika pamoja. Wafuasi wanashangaa kwa kutokewa na
Bwana kwani walikuwa na woga sana. Wamekusanyika pamoja siyo kutokana na upendo waliokuwa
nao kati yao, la hasha, bali kutokana na woga, kwa vile wanaye adui mmoja wanayemwogopa
yaani wayahudi.
Angalia watu wengine wanaotembea nje, wanawaacha tu hawa wafuasi
wajifungie humo chumbani, wao hawana wasiwasi wowote kwani ni kesi binafsi ya mitume
walioingiwa na wasiwasi kutokana na yaliyotokea. Hawa wanao woga kwa vile hawajamwona
Bwana mfufuka na kuhuishwa na roho ya mfufuka, hivi wanao woga. Woga huo unawapata
pia wakristu wowote katika jumuia kama endapo wanakuwa hawana mang’amuzi ya Kristu
mfufuka. Hali hiyohiyo inaweza kumkumba kila mkristu mkereketwa na Kristu kama anakosa
mang’amuzi ya Kristu mfufuka katikati ya ndugu zake.
Woga huo wa Mkristu unatokana
na mambo mawili: Mosi, kuogopa kifo. Mkristu aliyemwona Kristu anayeingia katika utukufu
wa Baba hawezi kuwa na woga wowote ule wa kifo. Anaweza kuwa na woga wa homa, ugonjwa,
mateso, lakini siyo wa kifo. Mtu huyo atasubiri kama “mlinzi akeshavyo akisubiri kuchomoza
kwa jua la asubuhi”.
Kuingia kwake makaoni kwa Baba yake ambako ni lengo la
wote, hakuwezi kumpatia woga wa kifo. Hata kama woga huo unabaki kutokana na kuachana
na wapenzi wake na vitu mbalimbali ambavyo Mungu ametupatia. Kwa hiyo hapa unauona
woga wa wanafunzi, ambao walikuwa bado hawajamwona Kristu mfufuka.
Woga wa
pili, unakuwa dhidi ya wengine ambao hawakuyapokea mapendekezo haya ya Yesu hadi wakataka
kumfifisha kabisa. Wenye woga aina hiyo hawawezi kuwa wanafunzi wa kweli, kwani Yesu
anawatuma wafuasi wake kama vile kondoo kati ya mbwa mwitu. Kama unao woga kwa mbwa
mwitu, basi ni bora kutoroka na kwenda mbali kujificha.
Kadhalika woga ni
ni kitu kibaya kupita kila kitu kingine katika imani, kwa sababu unawafanya wafuasi
wa dini kuwa wenye msimamo mkali, hawaambiliki, hawataki majadiliano, ni wagomvi,
ni wachokozi, wanapiga makelele, wanapenda zogo katika kuitangaza imani yao.
Kwa
sababu kama imani yao na wanachokisadiki kingekuwa cha ukweli na wanakiamini kwa dhati,
basi wasingekipigia makelele, badala yake wangekitangaza kwa furaha na kwa utulivu.
Pengine ingekuwa pia njia ya kujisaidia wao wenyewe ya kuuona mwanga wa Pasaka. Kwa
hiyo yatubidi tujiangalie sana, kwani woga unatuingiza katika hatari ya kujifungia
katika ukweli wetu usio na msingi wa kuchochewa tu na mapokeo wa mambo yale tuliyozoea
kuyatenda, tunakuwa viziwi mbele ya hali halisi na hivi kujikuta unajihami mbele ya
kosoo ya imani yako, na unakuwa mwoga wa mambo mapya.
Katika kipindi fulani
cha historia ya Wakristu, Kanisa lilikuwa na hofu kubwa sana wakati Biblia ilipokuwa
inamilikiwa na Waprotestanti. Kulikuwa pia woga wa demokrasia, na ule woga wa kukutana
na utamaduni au mila nyingine ngeni. Woga aina hiyo ni sawa na ule wa mitume wa kujifungia
ndani ya chumba. Yaani unakuwa na woga na mambo ya nje.
Huku kujitenga na kujifungia
ndani ya chumba katika nyumba moja, kuna maana pia ya kiteolojia: Yohane anataka kuonesha
kwamba mbele ya ulimwengu, wanafunzi wanajisikia katika mazingira mageni, wanayo thamani
ambayo si sawa na zile za ulimwengu. Yesu anasema, ninyi mpo katika ulimwengu lakini
si wa ulimwengu huu. Ndiyo maana wanakuwa na woga.
Aidha, endapo mmoja anajitangazia
kwamba amemwona Kristu mfufuka, anatangaza imani yake, hivi anaogopa kueleweka kuwa
ni kichaa, yaani ni mtu anayeishi nje ya ulimwengu, kwa sababu watu wamefungwa na
mtindo wa maisha ya ulimwengu huu hawaoni namna nyingine ya maisha. Kwa mfano Mtakatifu
Paulo anapozungumza juu ya ufufuko, watu wanamcheka na kumwambia waziwazi kwamba “juu
ya suala hilo tutakusikiliza tena wakati mwingine”.
Ni ngumu sana kushuhudia
imani yako hadharani. Hata mapadre, usiku wa Pasaka, hatuwi hata na uso wa furaha
wa kuona mwanga wa ufufuko. Kwamba Yesu yuko na alifika kusimama mbele ya wafuasi.
Yaani mwanzo mpya wa kudumu wa uwepo wa Yesu. Amefufuka na kuonesha mikono yake na
kuwa katikati yao. Anaonesha mikono iliyofanya kazi na ubavu wake, hiyo ndiyo kadi
yake ya utambulisho. Mikono iliyotenda mema na kupigiliwa misumari na moyo wake uliochomwa
mkuki ilipotokea damu kuonesha maisha na maji kuonesha Roho mtakatifu, maisha yaliyomwagwa
duniani maisha ya Roho yaliyotolewa ulimwengu. Hii ndiyo ID ya Yesu.
Mazingira
ya pili, aliyotokea Yesu ni ya siku nane baada ya ufufuko. Tomasi hakuwepo pale alipotokea
Yesu mara ya kwanza. Huyu Tomasi anaitwa Didimo maana yake Pacha, “Walakini mmoja
wa wale Thenashara, Tomas, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. .. Basi,
baada ya siku nane wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomas pamoja. Akaja Yesu
na milango imefungwa akasimama katikati , akasema, “Amani iwe kwenu.”(Yoh. 20: 24,
26). Mwinjili anasisitiza sana jina hili Pacha (Didimo). Yaonekana kuwa huyu ndiye
pacha wa kila mmoja wetu. Kwa sababu hata sisi tutapita safari hiyohiyo ya jinsi ya
kumfuata Kristu mfufuka.
Katika Injili, Thomasi anajitokeza mara tatu: Mara
ya kwanza ni pale Yesu anapotaka kwenda Yudea, alikokufa Larazo, Thomas anasema twende
tukafe sote huko: “Basi Tomas, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, “Twendeni
na sisi, ili tufe pamoja naye.” (Yoh. 11:16). Kwa hiyo ni kweli Tomasi anayo mang’amuzi
ya kifo tu, bali mang’amuzi ya ufufuko hana kwa sababu hajayashuhudia. Amebakiwa na
wazo lake lilelile, “Twendeni tukafe naye”. Nafasi nyingine ni kwenye karamu ya mwisho,
pale Yesu anapowaambia wanafunzi kwamba kule ninakoenda ninyi mnafahamu njia. Tomasi
anasema, sisi hatujui unakoenda, tutawezaje kuijua njia? “Nami niendako mwaijua njia.”
Tomas akamwambia, “Bwana, sisi hatujui uendako, nasi twaijuaje njia?” (Yoh. 14:4-5)
Huyu ndiye ndugu yetu Tomas, pacha wetu (Kurwa), kwa sababu anataka kujua. Kuna wakristu
wengi wanaopata taabu ya kuelewa mambo yote katika imani. Anaye pacha wa Tomasi atauliza,
“utuoneshe njia.” Kwani baada ya kuuliza Yesu anaweza kujieleza: “Mimi ni njia, na
kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” (Yoh. 14:6).
Hebu
tuangalie ni katika vipengee vipi Tomas anaweza kuwa ni pacha wako. Hoja ya mojawapo
yaweza kuwa Tomas alikuwa haelewi ni kwa nini wenzake wamejifungia chumbani. Yeye
ameondoka na kwenda kuzubaa sijui wapi kwa sababu hajisikii kuwa na woga wowote ule.
Katika kipengee hiki, Tomas ni pacha au kurwa wa mtu yule ambaye hajisikii kuwa wa
maana au bora zaidi kuliko wengine, yaani, haelewi ni kwa nini wengine wamejifungia
ndani.
Ni dhahiri kwamba Tomas siyo pacha wa wale wanaojitenga na jumuia ya
kikristu kwa sababu labda wanachekwa na kudharauliwa na wengine; wanaojisikia bora
zaidi na kuwahukumu wengine wasio katika jumuia au hata wanaowahukumu wale walio katika
jumuia kwamba ni waovu kuliko wengine, au kama wale wanaoacha dini yao na kuingia
nyingine.
Tomas hahukumu, wala kudharau wengine bali yawezekana anajiona kama
amedanganyika kidogo au amekwazika na jumuia ile. Yaani ni kama wakristu wale wanaoona
ndani ya kanisa kuna makwazo au mambo ya aibu, hivi wanajisikia kukwazika na kuteseka
mioyoni mwao. Hivi wanaona ni bora kujiweka kidogo pembeni.
Aina ya nyingine
ya kuwa pacha wa Tomas ni pale wale ambao wamedanganyika na muundo wa kanisa, na uendeshaji
wa mambo ya kanisa, kukosa mpango mzuri. Hakuna uinjilishaji wa kutosha, au kuna utawala
wa kibabe, kuna kujionesha ukuu unaotegemea mali, na hivi wanaona afadhali kujiepusha
kidogo. Waumini wasioamini kama mambo yanaweza kubadilika katika kanisa. Hawa ni pacha
wa Tomas.
Anapofika Tomas wenzake wanamhabarisha: “Tumemwona Bwana.” Kwa tamko
hili walikuwa wanataka kummweleza kwamba mambo yamebadilika, si kama alivyodhani au
kama alivyoyaacha. Tomas anataka kuhakikisha yeye mwenyewe kama kweli mazingira aliyoyaacha
yamebadilika.
Hapa sasa tunakutana na pacha mwingine, yaani wale wanaotaka
kuhakikisha kwa kuona na kugusa. Pacha wa Tomas ni wale wasiomwona Yesu wa Nazareti
lakini wameitwa kumwamini ili kumshuhudia kwa ndugu zao. Pacha ni wale wasioelewa.
Yaani hao pia wameitwa ili kuelewa lakini wanayo namna mbili ya kuelewa. Kimwili,
kuamini kwao ni kama kule Tomas, lakini ndani yao kuna haja na hamu ya kuamini ambayo
wanataka kuihakikisha.
Aliye na mang’amuzi haya ya ndani, ajue kwamba Tomas
ni pacha wake. Na kwamba tusiwe na woga wa kuungama mashaka yetu ambayo ni kama ya
Tomas, kama tunaweza kugusa kama Tomas hatuwezi kuwa na mashaka. Lakini kugusa huko
kwetu hakuwezekani.
Kwa hiyo ni vyema kabisa kuwa ndani yetu tunaye huyo pacha
wetu Tomas wa kuona mashaka kwamba huyo aliyetoa maisha kwa kufa kwake kama mtumwa
ameingia katika utukufu wa Baba. Kwa hiyo fundisho kuu tunalopata hapa kwa huyu pacha
wetu ni hili: Yesu anapofika siku ya nane anaonesha majeraha yake na anamwita Tomas
kuja kuhakikisha.
Huo ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kuweka mikono yetu ubavuni
pake. Kualikwa na Yesu Mfufuka kuweka mikono yako ubavuni mwake maana yake pale unapoweka
mikono yako, shughuli zako zote, na hasa ukijiweka wewe mwenyewe, kujiaminisha na
kujitoka kabisa maisha yako kwa upendo kama ya Yesu hapo umeingia katika ulimwengu
wa Mungu na wa utukufu wa ufufuo.
Upacha mwingine na Tomas ulio mzuri sana,
ni pale Yesu anapomwalika Tomas kuyatupa maisha yake kwenye mapendekezo ya mwalimu:
“Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni
mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.” (Yoh. 20: 27), naye Tomas anapojibu:
“Bwana wangu na Mungu wangu!” (Yoh. 20:28). Hilo ni ungamo la imani katika Mungu wa
kweli imani inayojidhihirisha katika ufufuko wa Kristu. Imani kwa Mungu anayetoa maisha
yake kwa ajili ya upendo.
Tomas aliyekuwa na mashaka, ndiye wa kwanza kushuhudia
imani iliyo safi ya wakristu wa kwanza. Ni yeye aliyeona uthibiti wa msulibiwa katika
ufufuko. Haamini juu ya Mungu anayeadhibu, anayezawadia, anayewapenda wema tu, amemwamini
katika Kristu aliyetoa maisha Mungu wa kweli ambaye hawezi kuwa mwingine isipokuwa
yule aliyesulibiwa kwa ajili ya upendo.
Uhakika kwamba ameona na kugusa mikono
na ubavu wa Mungu, uhakika ule anaweza kuwa nao tu kwa mtazamo wa imani. Mtazamo
unaotakiwa kuufungua daima pamoja na jumuia. Sisi tunasikia sauti ya Bwana na katika
mkate wa Ekaristi sisi tunagusa mapendekezo yake ya maisha ya kujifanya mkate kwa
ajili ya kutupenda.