Yohane XXIII ni mtoto wa mkulima aliyeleta mageuzi makubwa ndani ya Kanisa!
Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane
Paulo II kuwa ni Watakatifu, Jumapili ijayo tarehe 27 Aprili 2014, Baba Mtakatifu
Francisko ametuma salam na ujumbe wa matashi mema kwa waamini na wananchi wanaoishi
Kaskazini mwa Italia kwa Mwenyeheri Yohane XXIII kutangazwa kuwa Mtakatifu. Miaka
hamsini imekwisha kuyoyoma, lakini bado watu wengi wanamkumbuka kwa tabasamu na upole
wake kama Baba mwema!
Baba Mtakatifu anaialika Familia ya Mungu, Kaskazini
mwa Italia kumwimbia Mwenyezi mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi kubwa ya
utakatifu ambayo amelizawadia Kanisa; imani ambayo inabubujika kutoka katika uhalisia
wa maisha ya kawaida, kutoka kwa wakulima na wafanyakazi; familia zilizoonja upendo
na ukarimu wa Mungu, kiasi hata cha kuweza kushirikisha wengine katika hali ya kawaida
kabisa.
Mama Kanisa anawachangamotisha Watoto wake kujikita katika Uinjilishaji
Mpya pamoja na kuwasindikiza watu katika hija ya maisha yao ya kila siku, ili watu
waweze kupata Maji ya Uzima wa Milele. Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican
yamekuwa ni chanzo kikuu cha utakatifu wa Mwenyeheri Yohane XXIII na kwamba, ni furaha
kubwa tukio hili linamhusisha pia Yohane Paulo II, kiongozi aliyeleta mageuzi makubwa
katika maisha na utume wa Kanisa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba,
viongozi wa kiraia wataweza kujenga na kudumisha udugu na mshikamano.
Haya
ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko yaliyoandikwa kwenye Gazeti la "Eco de Bergamo",
gazeti ambalo Papa Yohane XXIII alishiriki kwa kuandika makala kwenye gazeti hili.