Ushuhuda wa utakatifu wa maisha, kadiri ya wale walioishi nao karibu!
Monsinyo Battista Angelo Pansa ni kati ya wataalam wa maandishi na historia ya Baba
Mtakatifu Yohane XXIII, ambaye ameonesha jinsi ambavyo Papa Yohane XXIII tangu akiwa
kijana alitamani sana maisha ya Upadre, kwa ajili ya kuwasaidia maskini katika maisha
yao ya kiroho.
Ni Papa aliyeanza kuonesha cheche za mageuzi katika maisha
na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Akatembelea Hospitali na Magereza ya
Roma ili kukutana na kuzungumza na wagonjwa pamoja na wafungwa. Aliithubutu kuanzisha
maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, akasafiri kwa Treni hadi Assisi na
Loreto kunako Mwaka 1962.
Alikuwa ni kiongozi aliyesimama kidete kulinda na
kutetea misingi ya haki, amani, utulivu na maendeleo ya wengi. Alikuwa na Ibada kwa
Bikira Maria aliyemsindikiza daima katika maisha na utume wake. Kwa wasaidizi wake
wa karibu aliwataka kupiga magoti mbele ya Sakramenti kuu na wala si kwake!
Monsinyo
Marco Frisina ambaye kwa miaka thelathini amekuwa ni kiongozi mkuu wa kwaya ya Jimbo
kuu la Roma anasema, maisha ya Mwenyeheri Yohane Paulo II yamejikita katika imani
na sanaa ni kiongozi aliyependa muziki na kwamba, kwa njia ya muziki, ujumbe wa Neno
la Mungu ulikuwa unawafikia wengi.