Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Huruma
ya Mungu!
Tunaendelea tena katika tafakari yetu masomo Dominika ya II ya Pasaka mwaka A. Ni
kipindi cha furaha kwa sababu ya ushindi dhidi ya kifo kwa njia ya ufufuko. Neno la
Mungu, linakazia na kuahidi furaha ya kweli kwa wale ambao hata kama hawakumwona Bwana
wanayo imani na tumaini la kweli katika yeye.
Katika Somo
la kwanza, kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume latuonesha furaha na tabia ya
jumuiya ya kwanza ya Yerusalemu. Kwa nini tunaoneshwa jambo hilo? Ni kwa sababu tunaalikwa
kuishi mtindo uleule wa jumuiya ya mwanzo katika mazingira yetu. Mambo msingi ya Jumuiya
ya I yalikuwa utii na usikivu wa watu kwa Neno la Mungu lililohubiriwa na Mitume.
Aidha waliweka mali yao na moyo wao pamoja kwa faida yao na kasi ya Injili.
Ili
kuimarisha mambo haya waliadhimisha pamoja Ekaristi Takatifu na kusali pamoja kwa
upendo. Mambo haya msingi yalifungamana na furaha, uchangamfu, ushirikiano ambavyo
vilikuwa vivutio kwa jumuiya nyingine nje ya Yerusalemu. Ndiyo kusema waliishi na
kukishuhudia kile walichohubiri katika maisha yao, yaani waliuishi ufufuko ambao ndilo
chimbuko la haya yote.
Mpendwa msikilizaji, wito kwetu hivi leo katika jumuiya
zetu ni kuanza polepole kupalilia nguvu ya ufufuko, ndiyo kusema tunaalikwa kushuhudia
daima kwa maisha yetu yakuwa Kristu ni mfufuka. Mpendwa, katika mantiki hiyo katika
jumuiya zetu lazima tabia za jumuiya ya kwanza zijitokeze na kukua na hivi kuwa kielelezo
cha mapendo kwa watu wa mataifa. Yafaa kukomaza ile tabia ya kushirikishana tulichonacho
hata kama ni kidogo. Tujifunze kuwa na kile kinachotufaa na kinachobaki kiwe kwa ajili
ya wale waliowahitaji katika jumuiya zetu.
Kumbuka usemi wa Mtakatifu Basil
akisema “kama mmoja wetu angechukua kwa ajili yake kinachohitajika na kingine kikawa
kwa ajili ya ndugu yake maskini, basi kusingekuwa na tajiri wala maskini katika jumuiya”.
Hii ni falsafa ya mgawanyo sawa ambayo tungepaswa kuifikia kama kweli tunataka kumfuasa
Bwana kwa ukamilifu! Mpendwa msikilizaji inaonekana kuna ugumu katika kushirikishana
mali tulizonazo, na hasa kuwapeni maskini, je toka tukiamini na kuendelea katika ugumu
huu twaweza kusema tunaishi na tunashuhudia ufufuko? Tafakari sana jambo hili!
Katika
somo la Pili toka barua ya kwanza ya Mtakatifu Petro tunakumbushwa siku ya ubatizo
wetu. Kwa njia ya ubatizo tulipata kuingia katika furaha isiyo na mwisho. Ndiyo kusema
Mt Petro anataka hata kama kuna madhulumu na taabu mbalimbali tusisahau furaha ya
milele. Anasema mateso ni ya kitambo kidogo tu na baadaye yanapita cha msingi ni kutazama
mbele tukiendelea kukua katika neema ya ubatizo.
Mtakatifu Petro anatukumbusha
kuwa mkristu katika ulimwengu huu ni mgeni na hivi yuko safarini kwenda nchi ya ahadi
yaani mbinguni. Tunakumbushwa kuwa hakuna mateso yanayoweza kuzima moto wa furaha
na mapendo uliowashwa wakati wa ubatizo. Wakristo ni kama dhahabu ambayo ili itengeneze
kitu cha thamani lazima ipitie moto ili ichomwe na kusafishwa tayari kwa kito cha
thamani. Katika somo la Injili, hali ya maisha ya jumuiya inajionesha wazi. Wanafunzi
wako pamoja ingawa wanahofu! Bwana anawakuta wakiwa pamoja na kuwatakieni amani. Anawaonesha
alama za madonda na wanafurahi na kusema tumemwona Bwana! Ni katika jumuiya hiyo Bwana
anawavuvia Roho Mtakatifu ili wapate kuondolea dhambi. Ni siku hii anaweka sakramenti
ya kitubio katika Kanisa na kisha anawatuma wakaende kutangaza habari njema. Kumbe
Toba ni mlango wa kazi ya kimisionari, ni mlango wa imani, ni mlango wa wokovu. Analikabidhi
kanisa ufunguo wa kufunga na kufungua katika mambo yamhusuyo Mungu katika uhusiano
wake na mwanadamu. Jumuiya wakati fulani zinakuwa na watu walio na mashaka katika
imani. Hali hii inajionesha leo pia. Ndiyo kusema, kumbe Mtume Tomaso ambaye hakuwapo
pamoja na wenzake siku ya kwanza haamini, bado ana mashaka kuhusu ufufuko! “Siamini
mpaka nitie vidole vyangu katika makovu ya Bwana! Baada ya siku nane tukio hilo la
kitaalimungu, Bwana anawatokea tena Mitume na wakati huo Tomaso yupo. Bwana anamwambia
lete mikono yako na uweke kidole chako katika ubavu wangu na usiwe asiyeamini! Tomaso
anajibu, Bwana wangu na Mungu wangu! Mpendwa, Mtume Tomaso anapokiri udhaifu wake
anatufundisha kuwa watu wa Imani na unyenyekevu mkubwa na hivi baada ya ufufuko hakuna
mashaka tena kinachobaki ni kwenda kutangaza habari ya furaha kwa mataifa. Mpendwa
leo hii wapo watu wa namna hii katika jumuiya zetu, kumbe wanaalikwa na Bwana kusadiki
pasipo kuona, na kwa namna hiyo Bwana anatangaza heri kwa wasioona wakasadiki na si
kwa wanaosadiki kwa sababu ya kuona. Mwishoni mwa sehemu ya Injili ya Dominika hii,
Mwinjili anatuambia pia zipo ishara nyingi ambazo hazikuandikwa na hivi mtu asishangae
ishara nyingine ambazo hazimo katika Biblia lakini ni muhimu kwa imani yetu na maisha
ya Kanisa. Nakutakieni furaha tele katika kipindi chote cha Pasaka na Mungu azidi
kuwa nawe, nawe ukitekeleza mapenzi yake katika Jumuiya kama Jumuiya ya kwanza ya
Waamini. Tukutane tena Dominika ijayo. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa
kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.