2014-04-25 09:54:31

Msiogope kumshuhudia Kristo katika ukweli na uhuru kamili!


Mama Kanisa, Jumapili ya pili ya Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Huruma ya Mungu anawatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa ni Watakatifu, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Kituo cha Televisheni cha Poland, Telewizja Polska (TVP) anasema kwamba, Mwenyeheri Yohane Paulo II alikuwa ni kiongozi mashuhuri na mchapakazi; aliyeonesha dira na mwongozo kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ni kiongozi aliyewachangamotisha waamini kumfungulia Kristo malango ya maisha yao. Papa Yohane Paulo II akawa ni mwamini wa kwanza kumfungulia Kristo milango ya maisha ya: Jamii, tamaduni, sera na mikakati ya kiuchumi na kijamii, dhamana aliyoitekeleza kwa nguvu ya kweli za Kiinjili.

Mwenyeheri Yohane Paulo II alileta mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa, kiasi cha kuwashangaza wengi. Alishuhudia yote haya kwa njia ya imani thabiti, mapendo kamili, ushupavu wa kitume, utu wema na mfano bora wa maisha yake. Alithubutu kuwajengea Wakristo uwezo wa kuwa na ujasiri wa kutoogopa kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa maneno machache, Waamini wanaalikwa kutoogopa kushuhudia ukweli ambao ni kielelezo cha uhuru kamili katika maisha ya mwanadamu.

Karol Wojtyla alijitoa bila ya kujibakiza kwa Kristo, nchi yake ya Poland na baadaye akajielekeza zaidi katika huduma kwa Kanisa la Kiulimwengu aliposhiriki katika maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Tarehe 16 Oktoba 1978 akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, akawa kweli ni Baba wa Mataifa katika lugha, jamaa na tamaduni, akawa yote katika wote.

Baba Mtakatifu Francisko anaishukuru kwa namna ya pekee Familia ya Mungu nchini Poland kwa kulizawadia Kanisa, Mwenyeheri Yohane Paulo II aliyewatajarisha wengi kwa uwepo na ushuhuda wake na anaendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wa Kanisa. Maneno, maandishi, vitendo na mtindo wake wa huduma kwa Kanisa ni mambo yanayopaswa kuendelezwa. Alijitahidi kumwilisha ndani mwake mahangaiko makubwa kwa njia ya matumaini thabiti, akajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Mkombozi wa binadamu na kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Poland inaendelea kuwa ni chemchemi ya nguvu ya: imani, sala, upendo na maisha ya Kikristo. Inapambana na changamoto kubwa katika maisha na utume kwa familia, kwa vijana, maskini na maisha ya Kipadre na kitawa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kutangazwa kwa Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II, italeta ari na mwamko mpya katika maisha ya kila siku na udumifu katika maisha na utume wa Kanisa nchini Poland.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, panapo majaliwa, kunako Mwaka 2016 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, atapata fursa ya kutembelea Poland kwa mara ya kwanza, ili kushiriki katika tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana. Baba Mtakatifu anatumia fursa hii kuwashukuru waandishi wa habari na watangazaji wote watakaochakarika kuwatangazia watu yale yatakayojiri katika Ibada ya kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa Watakatifu, Jumapili tarehe 27 Aprili 2014.







All the contents on this site are copyrighted ©.