2014-04-25 09:53:07

Kanisa linasimikwa katika furaha inayoshuhudiwa na Jumuiya ya waamini!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, jioni tarehe 24 Aprili 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani baada ya Mama Kanisa kumtangaza Mwenyeheri Padre Josè de Anchieta, Mtume mwaminifu wa Brazil kuwa Mtakatifu.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa waamini kutolea ushuhuda wa furaha inayobubujika baada ya kukutana tena na Kristo mfufuka anayewakarimia amani na maisha tele, tayari kufukuza giza la wasi wasi na hofu ya Wayahudi. Waamini wanapokutana na Yesu, wanapaswa kufurahia na kuwa na kiasi kwa kukutana na Yesu Kristo Mfufuka.

Ni rahisi kwa waamini wengi kujitumbukiza katika imani tepetevu ili kuwa na uhakika wa maisha yajayo badala ya kujenga imani na matumaini kwa Kristo Mfufuka aliyeshinda dhambi na mauti. Ni rahisi kwa waamini kuzama katika ndoto badala ya kuonesha unyenyekevu kwa Kristo Mfufuka anayewaalika na kuwatuma, badala yake, wanajikuta wanajitenga na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, Mitume wa Yesu waligubikwa mno na wasi wasi kiasi hata cha kushindwa kufurahia uwepo wa Kristo. Hii ndiyo hali halisi hata kwa Wakristo wa nyakati hizi.

Baba Mtakatifu anasema, Mitume waliendelea kufanya miujiza kwa nguvu ya Yesu Mfufuka, kiasi cha kuwaponya watu ambao waligeuka na kuwa ni mashahidi wa furaha ya ufufuko wa Kristo, matendo makuu ya Mungu. Mtume Petro aliyekuwa mwoga, anapata ujasiri wa kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, kikolezo muhimu cha kukua na kukomaa kwa Kanisa linaloendelea kutolea ushuhuda wa Ufufuko wa Kristo. Kanisa linasimikwa katika furaha inayoshuhudiwa na Jumuiya ya Waamini katika Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu anasema, waamini wanayo dhamana ya kuwashirikisha jirani zao Injili ya Furaha, ili kugundua maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Mtakatifu Josè de Anchieta, alibahatika kuwashirikisha wengine ile furaha iliyokuwa inabubujika kutoka katika undani wa maisha yake.

Ni kijana aliyetumwa akiwa na umri wa miaka kumi na tisa nchini Brazil, akabahatika kutekeleza utume wake kwa Kristo na Kanisa lake, akawa ni mwanga angavu katika maisha na ushuhuda wake pamoja na kumtegemea Bikira Maria. Alikuwa ni mhubiri mkuu wa amani iliyokuwa inabubujika kutoka katika Neno la Mungu pamoja na kushuhudia kwamba, Yesu amfufuka kweli kweli!







All the contents on this site are copyrighted ©.