2014-04-25 15:42:33

Jitahidini kuzikabili changamoto za maisha kwa njia ya ushuhuda makini, mafundisho ya Kanisa na kweli za Kiinjili!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 25 Aprili 2014 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, linaloundwa na Botswana, Swaziland na Afrika ya Kusini, ambalo linaendelea na hija ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano hapa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anawashukuru Maaskofu kwa kumshirikisha imani na utume wa kutangaza Injili ya Kristo Kusini mwa Afrika, eneo ambalo linaendelea kukua na kukomaa zaidi katika imani, matunda ya kazi za kimissionari. Katika kipindi cha miaka mia mbili, Kanisa Katoliki Kusini mwa Afrika limeendelea kuwekeza katika huduma kwenye sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Kazi ya Uinjilishaji inaendelea kwa kasi na ari kuu.

Baba Mtakatifu anasema, licha ya magumu na changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa kutokana na umbali, uhaba wa rasilimali fedha na watu pamoja na kukosekana kwa huduma za Kisakramenti kutokana na uhaba wa Mapadre, lakini Kanisa bado linaendelea kucharuka. Juhudi zinaendelea kufanyika kwa ajili ya kuwatayarisha Mashemasi wa kudumu, ili kusaidia sehemu ambako kuna uhaba wa Mapadre, juhudi ambazo zinapaswa kuimarishwa na majiundo makini kwa Makatekista wanaoshiriki kutoa Katekesi kwa vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa halina budi kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa utoaji wa huduma kwa: wajane, familia tenge pamoja na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi; wengi wao wakiwa ni wale walioathirika kutokana na ugonjwa wa Ukimwi. Huduma hii kwa sasa inatolewa na Kanisa kwa kusua sua kutokana na kupungua kwa misaada kutoka nje. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wafadhili wataendelea kusaidia juhudi hizi.

Baadhi ya changamoto zinazolikabili Kanisa Katoliki Kusini mwa Afrika ni: uhaba wa miito ya Kipadre na maisha ya kitawa; makundi makubwa ya Wakatoliki wanaokimbilia kwenye madhehebu mengine ya Kikristo, Utoaji mimba; talaka na ndoa nyingi kuendelea kuvunjika kiasi cha watoto kuishi katika mazingira ya wasi wasi na ukosefu wa usalama; dhuluma na nyanyaso dhidi ya wanawake na wasichana.

Matatizo yote haya yanahatarisha utakatifu wa maisha ya ndoa na familia; amani na utulivu ndani ya familia na jamii katika ujumla wake. Hapa Makleri na watawa anasema Baba Mtakatifu Francisko wanapaswa kutoa ushuhuda makini wa Mafundisho adili ya Injili, kwa kufundisha ukweli unaosindikizwa na sala, mang'amuzi pamoja na huruma kwa wahusika.

Baba Mtakatifu amewapongeza Maaskofu Kusini mwa Afrika kwa kuonesha mshikamano wa dhati na watu wasiokuwa na fursa za ajira, changamoto kwa Kanisa kuwasaidia kwa hali na mali kadiri ya uwezo uliopo, kwa kutambua kwamba, hakuna umaskini mkubwa kama ule wa kutomfahamu Kristo. Hapa kuna haja ya kutafuta mbinu mpya ya kukutana na Kristo kwa kuwa na uelewa mkubwa wa imani.

Upungufu wa Waseminari na Mapadre anasema Baba Mtakatifu ni changamoto kubwa katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Kuna haja ya kuhamasisha miito, kuwa makini katika kuchagua vijana wanaotaka kuanza masomo ya Ukasisi sanjari na kuwatia moyo wa kibaba wale ambao wako kwenye nyumba za malezi pamoja na kuwasaidia katika miaka ya kwanza kwanza baada ya Upadrisho.

Baba Mtakatifu anaipongeza Familia ya Mungu Afrika ya Kusini kwa kukua na kuongezeka, changamoto ya kuendelea kuziimarisha kwa njia ya Tafakari ya kina ya Neno la Mungu, maisha ya Sala pamoja na kupokea Sakramenti za Kanisa. Waamini wanapaswa kugundua ndani mwao umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho kama chemchemi ya maisha ya neema.

Utakatifu na udumifu wa maisha ya ndoa ni mambo ambayo yanapaswa kutiliwa mkazo, kwa kutambua kwamba kwa Wabatizwa, ndoa ni agano la kudumu kati ya bwana na bibi na kwamba hii ni sadaka inayowataka wanandoa kudumisha uaminifu wao. Maandalizi ya wanandoa watarajiwa hayana budi kukolezwa na Mafundisho juu ya Ndoa yaliyotolewa na Mwenyeheri Yohane Paulo II pamoja na kuendelea kuwahamasisha vijana kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kufunga ndoa, ili hatimaye, waweze kuwa ni baba na mama katika familia.

Baba Mtakatifu anasema, utepetevu wa maisha adili miongoni mwa Wakristo kwa kwa kukosa uaminifu na matokeo yake watu kujikuta wakizama katika rushwa na ufisadi ni mambo yanayoleta athari kubwa ndani ya jamii. Jumuiya za Kikristo zinachangamotishwa kuwa ni kielelezo cha karama ya ukweli na uaminifu, wakisimama mbele ya Bwana wakiwa ni mikono na mioyo safi. Baba Mtakatifu anawahimiza Maaskofu kuendelea kushughulikia matatizo mengine ya kijamii kama vile wakimbizi na wahamiaji, ili waweze kuonja ukarimu kutoka katika Jumuiya za Wakristo.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mara baada ya kuadhimisha Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya miaka hamsini ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa Kusini mwa Afrika litajielekeza zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, kwa kutangaza kwa ari na moyo mkuu Injili ya Furaha. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kuiweka Familia ya Mungu Kusini mwa Afrika chini ya ulinzi na usimamizi wa Watakatifu wa Afrika na Bikira Maria, Malkia wa Afrika awaongoze katika kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza Watu wa Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.